Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Atoa Wiki 1 Kukamilishwa kwa Taratibu za Uwekezaji kwa Kampuni ya SIT
Apr 17, 2019
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wiki 1 kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Viwanda na Biashara kukamilisha taratibu za uwekezaji kwa kampuni Sugar Investment Trust (SIT) ya Mauritiusambayo imecheleweshwa kuwekeza katika uzalishaji wa sukari tangu mwaka 2017.

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayoleo tarehe 17 Aprili, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo Bw.Gansam Boodramaliyeongozana na Balozi wa Mauritius hapa nchini Mhe. Jean Pierre Jhumun.

Katika mazungumzo hayo Bw. Boodramameeleza kuwa yupo tayari kulima ekari 25,000 za mashamba ya miwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari na kwamba uwekezaji huo utawezesha kuzalishwa kwa tani 125,000 za sukari, ajira za kudumu 3,000 na ajira za muda 5,000 lakini amekwama kuendelea kutokana na kusubiri majibu ya Serikali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu upatikanaji wa eneo la uzalishaji wa miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.

Mhe. Rais Magufuli ameagiza ufanyike uchambuzi wa haraka katika maeneo ya Bonde la Mto Rufiji Mkoani Pwani, Eneo la shamba la Mkulazi Mkoani Morogoro na eneo la Kibondo Mkoani Kigoma ili mwekezaji huyo apatiwe na kuanza mara moja uwekezaji kwa kuwa nchi inahitaji kuongeza uzalishaji wa sukari utakaomaliza upungufu wa tani zaidi ya 100,000 ambazo kwa sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Edward Mhede kufuatilia makubaliano ya ushirikiano katika uvuvi kati ya Tanzania na Mauritius ambayo hayajatiwa saini tangu mwaka 2017 licha ya wawekezaji wa Mauritius kuonesha nia ya kutaka kuwekeza katika uvuvi na viwanda vya samaki.

Mhe. Balozi Jhumun amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa Mauritius inao uzoefu mkubwa katika uvuvi na viwanda vya samaki na kwamba kwa kuitikia wito wake wa kuhamasisha wawekezaji kuja hapa nchini, amefanikiwa kupata kampuni zilizotayari kufanya uwekezaji huo baada ya makubaliano kati ya Tanzania na Mauritius kutiwa saini.

Mhe. Rais amezionya taasisi za Serikali kikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kutoharakisha taratibu za kuwawezesha wawekezaji kuwekeza na amemhakikishia Mhe. Balozi Jhumun kuwa atafuatilia kuhakikisha uwekezaji wa kampuni ya SIT unafanyika.

“Ndugu zangu watendaji wa Serikali badilikeni, achene kukwamisha wawekezaji, fanyeni maamuzi na kama yanawashinda toeni taarifa kwenye mamlaka za juu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

17 Aprili, 2019

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi