Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Apongezwa kwa Hatua Mbalimbali Anazozichukua
Oct 25, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo

Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Manispaa na Majiji, Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri wamempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi anayoyafanya katika kutetea rasilimali za nchi pamoja na kuwatetea wanyonge.

Pongezi hizo zimetolewa leo Mjini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri  kwa niaba ya viongozi hao alipokuwa akifunga Warsha ya Kitaifa Juu ya Maboresho ya Huduma za Umma na Ugatuaji wa Madaraka kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa uliohusisha  Wakuu wa Mikoa Saba, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Manispaa na Majiji pamoja na Wakurugenzi kutoka TAMISEMI na Ofisi ya UTUMISHI.

“Tunampongeza Rais Magufuli kutokana na maamuzi makubwa anayoyafanya katika  sekta mbalimbali zikiwemo sekta za madini, elimu, bandari pamoja na mapato ya nchi tangu alipoingia madarakani,” alisema Mwanri.

Aliendelea kwa kusema, katika kipindi chake cha miaka Miwili tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu ambapo leo mtoto wa kitanzania ana uhakika wa kusoma bila kulipa ada jambo ambalo halikuwepo hapo awali.

Mwanri amesema, Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele katika kutetea rasilimali za nchi kama vile makinikia ambayo kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikipoteza mamilioni ya fedha na kutajirisha makampuni kutoka nje huku ikiwaacha Watanzania wangali masikini.

Pia amesema kuwa, maamuzi ya Rais Magufuli juu ya urekebishaji wa sheria za madini sasa utawanufaisha Watanzania wote kwani pesa zitakazopatikana zitarudi kwa wananchi kupitia miradi mbalimbali itakayotekelezwa ikiwa nia pamoja na miradi ya maji, afya, elimu na ujenzi wa barabara.

Vile vile Mwanri amempongeza Rais Magufuli kwa namna ambavyo amekuwa akiisimamia sekta nzima ya mapato ambapo sasa nchi inakusanya fedha nyingi zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Viongozi hao wamesema wapo pamoja na Rais Magufuli, hivyo wamemtaka Rais kusonga mbele na kutosikiliza watu wachache wanaopinga juhudi zake kutokana na kukosa uzalendo wa nchi yao.

Leo imetimia miaka miwili tangu watanzania walipoamua kumchagua Rais John Pombe Magufuli kuwa Rais wao, ambapo Watanzania wote nchini walipiga kura na kumchagua mnamo Oktoba 25, 2015.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi