Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Apokea Mchango wa Milioni 125 Kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta, Akutana na Katibu Mtendaji SADC
Oct 09, 2018
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 08 Oktoba 2018, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kenya hapa nchini Mhe. Dkt. Dan Kazungu na kupokea hundi ya shilingi Milioni 125 kutoka kwa Raiswa Jamhuri ya KenyaMhe. Uhuru Kenyatta ikiwa ni rambirambi ya ajali ya MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 Septemba 2018 katika ziwa Victoria.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi rambirambi hiyo kwa Mhe. Rais Magufuli,Mhe. Kazungu amesema Wananchi wa Kenya wanaungana na Watanzania katika majonzi ya kuwapoteza watu228 na wengine kujeruhiwa.

“Mhe. Rais Uhuru Kenyatta amenituma nifikishe rambirambi hii kutokana na kuguswa na ajali hiyohasa ikizingatiwa nyinyi ni ndugu na jirani zetu,tumechangia fedha hizo kuonesha upendo kwani janga la Tanzania ni la Kenya pia” amesema Dkt. Kazungu.

Kwa upande wake Mhe. Rais Dkt. Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wa Kenya kwa kuguswa na ajali hiyo na ameahidi kuwa fedha hizo zitaelekezwa kuwasaidia wananchi wa visiwa vya Ukerewe ikiwa ni pamoja na kujenga hospitali kubwa yenye hadhi ya Wilaya.

“Mwambie Mhe. Rais kuwa nashukuru sana, tulipanga fedha tulizopata tujenge wodi za wagonjwa lakini sasa tumeamua tujenge hospitali kubwa yenye hadhi ya Wilaya, na kwa mchango huu tunaweza kuamua wodi moja tukaiita Wodi ya Kenyatta” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine,Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax.

Dkt. Stergomena Tax amesema amekutana na Mhe. Rais Magufuli kumpa taarifa rasmi kuwa Mkutano wa 38 wa SADC uliofanyika tarehe 17 – 18 Agosti, 2018 mjini Windhoek Namibiaumemteua Mhe. Rais Magufuli kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2018 hadi Agosti 2019, na kwa maana hiyo Mhe. Rais Magufuli ndiye atakuwa Mwenyekiti ajaye wa SADC kwa kipindi cha mwaka 2019/2020.

Dkt. Stergomena Tax amesema SADC inaendelea vizuri na kwamba katika ajenda zake imetilia mkazo maendeleo jumuishi ya viwanda na hivyo kuendana na sera ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Mhe. Rais Dkt. Magufuli amempongeza Dkt. Tax kwa kuteuliwa kwa mara ya pili kuwa Katibu Mtendaji wa SADC na pia amempongeza kwa kazi nzuri anazozifanya katika Jumuiya hiyo.

Mhe. Rais Magufuli amesema amepokea kwa heshima kubwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa SADC nakwamba yupo tayari kushirikiana na viongozi wenzake wa Jumuiya hiyo katika kutekeleza jukumu hilo.

“Nimepokea kwa heshima kubwa na nipo tayari kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na wenzangu” amesema Rais Magufuli.

Amesemanchi za SADC zina watu takribani Milioni 400 na hivyo kuwa fursa muhimu ya soko la bidhaa mbalimbali na kwamba kutokana na sifa zake Tanzania imeteuliwa kuwa mnunuzi wa dawa na vifaa tiba kwa nchi 16 za SADC kupitia utaratibu wa ununuzi wa pamoja.

Jaffar Haniu

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es salaam

08 Oktoba, 2018

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi