Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Amuapisha Naibu Mkurugenzi TAKUKURU
Aug 24, 2017
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Brigedia Jenerali John Julius Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Ikulu jijini Dar es salaam leo.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 24 Agosti, 2017 amemuapisha Brigedia Jenerali John Julius Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Hafla ya kuapishwa kwa Brigedia Jenerali John Julius Mbungo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi na Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Pamoja na kula kiapo cha kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Julius Mbungo amekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi nyenzo za kazi  Brigedia Jenerali John Julius Mbungo baada ya kumuapisha kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Ikulu jijini Dar es salaam leo.

Akizungumza mara baada ya kiapo Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi na ustawi wa jamii.

“Ukiangalia mambo makubwa tunayopambana nayo yanasababishwa na rushwa iliyosambaa kila mahali, watumishi hewa chanzo ni rushwa, dawa za kulevya ndani yake kuna rushwa, vyeti feki ndani kuna rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa, pembejeo za ruzuku ndani kuna rushwa na huko mahakamani nako ni rushwa tu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TAKUKURU kwa kazi iliyoanza kuifanya lakini ametaka juhudi zaidi ziongezwe ili watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza  Brigedia Jenerali John Julius Mbungo akila kiapo cha maadili ya Viongozi wa serikali baada ya kumuapisha kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Ikulu jijini Dar es salaam leo.

Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na taratibu za uchunguzi na uendeshaji wa mashitaka ya rushwa zinavyochukua muda mrefu na ametoa wito kwa viongozi wa TAKUKURU kufanyia kazi eneo hilo ili vita dhidi ya rushwa ionekane ikizaa matunda haraka.

“Tukifanikiwa kupunguza rushwa kwa angalau asilimia 80, nchi yetu itafanikiwa kutatua matatizo mengi, na ni vema mtambue kuwa hatua hizi tunazochukua zimeanza kuwavutia wafadhili wengi na wawekezaji.

“Na mimi nikiwa kiongozi wenu nimeamua kupambana na rushwa kikwelikweli, na ninawaomba nyote mshirikiane kuondoa rushwa katika maeneo yenu ya kazi” amefafanua Mhe. Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan,  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) Mhe. Angela Kairuki, Waziri wa sheria na Katiba Profesa palamagamba Kabudi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju, katibu Mkuu Kiongozi Balozi  John Kijazi, wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Brigedia Jenerali John Julius Mbungo baada ya kuapishwa kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Ikulu jijini Dar es salaam leo.

Kabla ya Mhe. Rais Magufuli kuzungumza, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Julius Mbungo ameshukuru kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine wa TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.

Nae Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela amewataka viongozi wote wa umma kuhakikisha wanajaza fomu za tamko la mali kwa wakati na pia amewataka kutoa ushirikiano kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma pale inapochukua hatua ya kufanya uhakiki wa taarifa zilizojazwa katika fomu hizo.

Kwa upande wake Waziri Anjellah Kairuki na Mkurugenzi wa Utawala wa TAKUKURU Bw. Alex Mfungo wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumteua Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na wamemhakikishia kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

24 Agosti, 2017

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi