Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06 Februari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Mhe. Filippo Grandi, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumhakikishia kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano na shirika hilo katika kutekeleza jukumu la kuhudumia wakimbizi.
Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi kutoka nchi mbalimbali baada ya kutokea machafuko katika nchi hizo, na imekuwa ikiwapa hifadhi na kuwaruhusu watumie rasilimali za Watanzania licha ya wakati mwingine kutopata misaada kutoka Jumuiya ya Kimataifa.
“Nchi yetu kwa sasa ina wakimbizi 350,000 waliopo katika maeneo mbalimbali wakiwemo 40,000 wa kutoka nchini Burundi, tunawapa hifadhi na wanatumia huduma za kijamii na miundombinu ya Watanzania katika maeneo wanayoishi.
Nimefurahi Mhe. Grandi anasema tutaendelea kushirikiana na kwamba sasa wapo tayari kusaidia gharama za kuhudumia wakimbizi pamoja na jamii katika maeneo wanayoishi wakimbizi, maana tangu miaka 10 iliyopita UNHCR imekuwa ikiahidi kutoa fedha za kusaidia wakimbizi lakini haitekelezi ahadi zake” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na dhamira njema ya kuwapa hifadhi wakimbizi na kuwapa uraia baadhi ya wakimbizi, Serikali inaendelea kuwahimiza kurejea makwao wakimbizi ambao katika nchi zao machafuko yamekwisha ili wakaungane na familia, ndugu, jamaa na kujenga nchi zao.
Kwa upande wake Mhe. Grandi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuendelea kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi kutoka nchi zenye matatizo mbalimbali, na amesema UNHCR inatambua mchango mkubwa ambao kwa miaka mingi Tanzania inautoa kuwapa hifadhi na kuwahudumia wakimbizi kutoka kwenye nchi zinazoizunguka ambazo zimekuwa na machafuko ya mara kwa mara.
Mhe. Grandi ameahidi kuwa UNHCR itahakikisha inatekeleza ahadi zake za kusaidia jukumu la kuwapa hifadhi wakimbizi, kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimekuwa vikifanya kazi kubwa ya kuhudumia wakimbizi hao kwa kuvipatia teknolojia na vitendea kazi pamoja na kusaidia jamii katika maeneo yanayokaliwa na wakimbizi.
Aidha, Mhe. Grandi ameomba radhi kufuatia Serikali ya Tanzania kukamata makontena yaliyoingizwa nchini yakiwa na nguo zinazofanana na sare za jeshi hali iliyolazimu nguo hizo kuchomwa moto, na kubainisha kuwa jambo hilo halitajirudia.
“Ilitokea kampuni moja ya Japan ilitoa msaada wa nguo kwa ajili ya wafanyakazi wetu, nguo zile kwa bahati mbaya zilikuwa zinafanana kama sare za jeshi, na tulizipokea ili tuzisambaze kwenye maeneo ambayo tunawahudumia wakimbizi, hili ni kosa, hatukupaswa kufanya hivyo na hatujawahi kufanya hivyo, lakini wakati mwingine vitu hivi vinatokea, namuomba radhi Mhe. Rais na namuahidi kuwa haitatokea tena” amesema Bw. Grandi.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Grandi kwa uungwana wake wa kuomba radhi kwa kitendo cha kuingiza nguo zinazofanana na sare za jeshi na amesema anaamini UNHCR haitarudia kufanya hivyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Februari, 2019