Na. Immaculate Makilika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameichangia timu ya Taifa ya mpira wa miguu (Taifa stars) kiasi cha fedha shilingi milioni 50, ambazo zitatumika katika maandalizi ya wachezaji hao ambao wanatarajia kuwa na mechi dhidi ya timu ya Lesotho.
Akizungumza leo Ikulu Jijini Dar es salaam, ambapo aliwaalika wachezaji wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu , viongozi wa mchezo wa mpira wa miguu pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Rais Magufuli amesema kuwa anaichangia fedha timu hiyo ili ifanye maandalizi mazuri yatakayosaidia timu hiyo kushinda dhidi ya timu ya Lesotho.
“Mimi nawachangia shilingi milioni 50, na fedha hizi zitumike kwa watu wanaotakiwa kwenda kufanya mazoezi ambayo ni maandalizi kabla ya kwenda kwenye mechi huko nchini Lesotho” alisema Rais Magufuli
Hata hivyo Rais Magufuli alisisitiza kuwa fedha hizo zinatakiwa kutumika na wacheza wa timu hiyo ya Taifa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi na viongozi wasitumie mwanya huo kutumia fedha hizo bila mpango uliokususdiwa.
“Nitashangaa sana ikiwa watu wanaoenda kwa ajili ya kufanya mazoezi watakua 30, alafu wasindikizaji 40” alisisitiza Rais Magufuli.
Ambapo, Rais Magufuli, amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia kusimamia vyema matumizi ya fedha hizo ili yaweze kuwasaidia wachezaji kwa maslahi ya Taifa.
Aidha, Rais Magufuli, amewaasa wachezaji hao wa timu ya Taifa kucheza mpira kwa ustadi na umakini mkubwa huku akisema watanzania wamechoka kuwa wasindikizaji katika mashindano na michezo mbalimbali, na hasa mchezo wa mpira wa miguu, badala yake timu hiyo inatakiwa kufanya mabadiliko hasa wakati huu ambao wamempata kocha Emmanuel Amunike kutoka nchini Nigeria anayeaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuisaidia timu hiyo ya Taifa.
“Timu yetu muuite Tanzania, nendeni mkacheze kwa umoja kama timu, mpira ni ajira, mkacheze vizuri ili muweze kufuzu kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), na wengine mtakuja kuwa wachezaji wa kimataifa” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewataka vongozi wa mchezo wa mpira wa miguu kutofanya ubadhirifu wa fedha, na kuvitaka viwanja vyote vya mchezo wa mpira wa miguu kutumia mfumo wa kielektroniki katika kukusanya mapato ili kuzuia mianya ya upotevu wa fedha.
Taifa Stars inahitaji kushinda mechi zake mbili za marudiano zilizobaki za Lesotho na Uganda ili kufuzu kushiriki katika fainali hizo.