Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Aapisha Wakuu wa Mikoa, Katibu Tawala wa Mkoa na Kamishna Jenerali Dawa za Kulevya
Jul 06, 2020
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06 Julai, 2020 amewaapisha Wakuu wa Mikoa 2, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya 1 na Katibu Tawala wa Mkoa 1, na pia ameshuhudia Wakuu wa Mikoa wakiwaapisha Wakuu wa Wilaya 9 Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma.


Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Kamishna wa Polisi Thobias Emir Andengenye kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Philemon Rugumiliza Sengati kuwa Mkuu wa Mkoa Tabora, Bw. James Wilbert Kaji kuwa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Bi. Mariam Perla Mmbaga kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu.


Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia kuapishwa kwa Kanali Mathias Julius Kahabi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Ismail Twahir Mlawa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. Albinus Mgonya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Bw. Wilson Samwel Negile Shimo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale na Bw. Abbas Juma Kayanda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu.


Wengine aliowashuhudia wakiapishwa ni Bw. Toba Alnason Nguvila kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhandisi Martine Ntemo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Bw. Lazaro Jacob Twange kuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, Bi. Jamila Yusuph Kimaro kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda na Bw. Salum Abdallah Kalli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu.


Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na Wakurugenzi wa Halmashauri walioteuliwa hivi karibuni ambao ni Bw. Elias Amede Ng’wanidako (Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya), Anastazia Tutuba (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same), Bw. Saad Mutambule (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha), Bw. Duncan Golden Thebas (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala) na Bw. Mwailafu Thomas Edwin (Mkurugenzi wa Mji wa Nanyamba).


Wengine ni Bi. Erica Epaphras Yegella (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara), Bw. Hassan Njama Hassan (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero), Bw. Kanyala Malima Mahinda (Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Ifakara) na Bw. Waziri Khachi Kombo (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo).


Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali walizopangiwa na amewataka kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia viapo vyao, taratibu na sheria na kushughulikia kero za wananchi, badala ya kuacha kero hizo zikisubiri kushughulikiwa na viongozi wa kitaifa.


Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. James Wilbert Kaji aliyekuwa Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na ameamua kumthibitisha kushika wadhifa huo kutokana na utendaji wake mzuri ambapo hivi karibuni alifanya operesheni katika Mkoa wa Arusha na kufanikiwa kukamata magunia 143 (sawa na tani 2.5) za bangi.


Pamoja na kumthibitisha Bw. Kaji, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua dhidi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Afisa Usalama wa Wilaya (DSO) na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OCCID) katika Mkoa wa Arusha ambako operesheni iliyoongozwa na Kamishna Jenerali Kaji imefanywa ilihali wao wapo.


Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Wakuu wa Mikoa, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu na viongozi wa Mkoa wa Dodoma.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
06 Julai, 2020

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi