Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 10 Oktoba, 2023 ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (Doctorate Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru kwenye hafla iliyofanyika New Delhi nchini India.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo, Rais Mhe. Dkt. Samia ameshukuru uongozi wa chuo hicho kwa heshima aliyopewa kwa kuwa ni mara yake ya kwanza kupewa heshima hiyo nje ya nchi baada ya kupatiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari kutoka katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
“Nilikuwa na nafasi lakini sikuwaza kuwa Rais wa Tanzania tena kama mtoto wa kike katika eneo linalotawaliwa na wanaume, nilisoma wakati nikifanya kazi na sikuwahi kufikiri kupata nyongeza katika jina kutoka katika chuo hiki ambacho kiko umbali mrefu kutoka nyumbani,” amebainisha Rais Dkt. Samia.
Aidha, Rais Mhe. Dkt. Samia ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wazazi wake kwa kuona umuhimu wa kuwekeza kwa mtoto wa kike, amekishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na watu wote waliomshika mkono na hivyo kumuwezesha kufika mahali alipo.
Katika hatua nyingine Rais Samia kupitia heshima hiyo amewatunukia watoto wa kike wa kitanzania, hasa wanaoishi kwenye mazingira magumu, huku akiwatia moyo kwamba hakuna lisilowezekana.
“Tuzo hii ninaitoa kwa wasichana wa kitanzania ambao wanaishi maeneo ya vijijini (remote parts of the country) nataka wajue ya kwamba kwa kufanya kazi kwa bidii na kujitoa kunasaidia kwani hakuna lisilowezekana,” ameongeza Rais Dkt. Samia
Rais Samia anakuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa shahada hiyo ya heshima na chuo hicho ambapo taarifa kutoka chuoni hapo zinasema kuwa, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969, ni viongozi wawili tu nje ya India, ambao wamewahi kutunukiwa shahada hiyo, ambao ni pamoja na Rais wa Russia Vladmir Putin, na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe.