Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Dkt. Mwinyi Atoa Rai kwa ZRCP Kuanzisha Mfumo Wezeshi Kwenye Biashara Zinazochipukia
Sep 17, 2024
Rais Dkt. Mwinyi Atoa Rai kwa ZRCP Kuanzisha Mfumo Wezeshi Kwenye Biashara Zinazochipukia
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akikabidhiwa Ripoti ya Utafiti wa Wazalishaji Wanaoibuka Zanzibar na Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Utafiti za Maendeleo ya Kijamii, Uchumi na Uchambuzi wa Sera Zanzibar (ZRCP), Prof. Mohammed Hafidh Khalfan wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Kituo cha Utafiti Masuala ya Kijamii Zanzibar (ZRCP) uliyofanyika leo 17-9-2024 katika ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al Bahar Mbweni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar.
Na Ikulu - Zanzibar

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar ina kila sababu ya kuanzisha mfumo wezeshi kwenye biashara zinazochipukia zenye uwezo wa kukua kwa haraka ili kustawisha maisha ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. 

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua mkutano wa tatu wa pamoja wa taasisi ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera za Kijamii na Uchumi Zanzibar (ZRCP) leo tarehe 17 Septemba, 2024 kwenye ukumbi wa hoteli ya Madinatul Bahri, Wilaya ya Magharibi B.

Amefahamisha kuwa Zanzibar ina wajasiriamali vijana wenye vipaji wanaochipukia kwenye ujasiriamali, hivyo ni muhimu kuwakuza kwa ajili ya uchumi jumuishi na endelevu wa Taifa. 

Pia Dkt. Mwinyi alisema, kuna umuhimu mkubwa wa kuwawekea mazingira bora na rafiki ili wavumbue biashara zenye faida kubwa na kuviendeleza vipaji vyao kwa maslahi mapana ya Taifa.

Alifahamisha, nchi nyingi duniani zikiwemo Uholanzi, India, Korea Kusini pamoja na nchi za Afrika kama Kenya, Tunisia, Afrika ya Kusini na Nigeria zimetumia mfumo huo ipasavyo katika kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii, kukuza utajiri wa nchi zao, kuongeza pato la taifa na kutengeneza ajira zenye maslahi makubwa. 

Rais Dkt. Mwinyi amezielekeza taasisi zilizoratibu mkutano huo, kuongoza mijadala na mada zitakazojadiliwa kwa umakini ili ziletee tija nchini kulingana na mazingira ya kiuchumi na biashara ya Zanzibar.

Aliwahakikishia wadau na washiriki wa mkutano huo kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuziimarisha Taasisi za kukuza Uchumi ili kuhakikisha vijana wanakuza taaluma zao na kushiriki kikamilifu katika kuvumbua na kuendeleza vipaji vyao.

Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi alitoa wito kwa taasisi za Serikali kuzitekeleza kwa vitendo sera na miongozo mbalimbali itakayoanzishwa na ile iliyopo yenye lengo la kusimamia utekelezaji wa maazimio ya kukuza vipaji vya wataalamu kupitia nyanja zote za ubunifu na teknolojia.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya Salum amesema utafiti unaofanywa na kituo cha ZRCP una lengo la kuweka msukumo wa kufanikisha malengo ya Serikali na kuleta mageuzi kwa kiasi kikubwa yanayotokana na sayansi na teknolojia kwa vile Zanzibar inakusudia kuanzisha soko la mitaji hivyo, ni vyema kuwa na namna bora ya kufuatilia matokeo yanayotokana na utafiti ili kufikia malengo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZRCP Juma Reli, amesema ZRCP imekusudia kuwa kituo bora chenye kutoa tafiti za hali ya juu na zenye manufaa kwa jamii katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuihakikishia Serikali kwamba kituo hicho kipo tayari kufanya kazi na Serikali kwa weledi, ukweli na uadilifu.

Mkutano huo wa siku mbili umewakutanisha pamoja wadau kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi, washirika wa maendeleo na taasisi za kimataifa, una lengo la kutafuta na kujadili namna bora ya kutumia teknolojia na utafiti ili kubaini changamoto na mwelekeo mpya wa kuwakuza wajasiriamali wanaochipukia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi