Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Prof. Mbarawa Abainisha Vipaumbele Ujenzi wa Miundombinu
Aug 04, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema vipaumbele vya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2022/23 vinakusudia kuhuisha uchumi wa nchi na kuwakomboa Watanzania wa ngazi zote.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Prof. Mbarawa amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kukamilisha ujenzi wa barabara za lami zinazounganisha mikoa yote nchini ili kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi katika sekta mtambuka.

Amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa km 3.2 Jijini Mwanza, kukamilisha Daraja la Wami linalounganisha Mkoa wa Pwani na Tanga, na Ujenzi wa Barabara za kupunguza msongamano na magari yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam na  Barabara za mzunguko jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa Serikali pia itaendelea na upanuzi wa Bandari za Dar es Salaam na Tanga, Ujenzi wa Meli katika Ziwa Victoria na Tanganyika, upanuzi wa viwanja vya ndege nchini na ujenzi wa nyumba za viongozi na watumishi wa umma katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tumejipanga kuhakikisha miradi hii tunayoitekeleza inazingatia thamani ya fedha na kuzalisha ajira kwa Watanzania wenzetu kadri inavyowezekana,” amesisitiza Prof. Mbarawa kwa wanahabari.

Aidha, Wizara imejipanga kuhakikisha inawezesha wakandarasi wazawa na wahandisi wanawake kupata kazi na utaalam ili kuwawezesha kushiriki na kuendeleza kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa nchi.

Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) sehemu ya kwanza inayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro (Km 300), Prof. Mbarawa amesema kuwa majaribio ya reli hiyo yanatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2022.

Akifafanua zaidi kuhusu upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam amesisitiza kuwa ujenzi wa gati namba 8-11 unaenda sambamba na upanuzi wa gati namba 1-2 katika Bandari ya Tanga ili kuziwezesha bandari hizo kufanya kazi kwa ufanisi.

Kuhusu utunzaji wa miundimbinu ya barabara na madaraja, Waziri Mbarawa amesema Wizara itaendelea kujenga mizani ya kisasa ili kudhibiti magari yanayozidisha uzito ili kuilinda miundominu hiyo.

Zaidi ya Km 1500 za barabara za lami pamoja na madaraja makubwa manne yanaendelea kujengwa katika Bajeti ya Sekta ya Ujenzi, wakati katika Sekta ya Uchukuzi ujenzi wa njia ya reli kipande cha Tabora – Isaka Km.165 na Tabora – Kigoma Km. 411 zinatarajiwa kuanza ujenzi wake.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi