Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Prof. Elisante Ole-Gabriel: "Utamaduni wa Kweli Unaanzia kwenye Fikra".
Aug 24, 2017
Na Msemaji Mkuu

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole-Gabriel akiongea na wadau wa masuala ya utamaduni toka baadhi ya nchi za Afrika Mashariki wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa siku tatu unaohusu kujadili mambo ya utamaduni baina ya nchi hizo unaofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Na Genofeva Matemu.

Washiriki wa kongamano la Utamaduni na Fasihi la Afrika Mashariki wametakiwa kuhamasisha jamii kwa kutumia utamaduni kama inta inayoshikamanisha watu kuwa wamoja kwa kuzingatia utamaduni wa kifikra kuanzia ngazi ya familia ili kuweza kutengeneza amani bila kujali tofauti zetu za kidini, kisiasa na kikabila.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel leo wakati wa ufunguzi wa Kongamano latatu la Utamaduni na Fasihi la Afrika Mashariki linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Natumaini baada ya kongamano hili la tatu kila mwanasemina atahamasisha amani kwa nguvu zake zote na kuifanya kuwa sehemu ya utamaduni wetu kwani nchi yoyote isiyokuwa na utamaduni ni rahisi kuparanganyika hivyo silaha yetu kubwa ni utamaduni utakaohimarisha amani na mshikamano katika jamii” amesema Prof. Gabriel

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Cuthbert Kimambo akiongea na wadau wa masuala ya utamaduni toka baadhi ya nchi za Afrika Mashariki wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa siku tatu unaohusu kujadili mambo ya utamaduni baina ya nchi hizo unaofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha Prof Gabriel amewataka washiriki wa kongamano hilo kuendelea kuelimisha na kuhamashisha watanzania kuwa na utamaduni wa kujisomea na kupenda kusoma mambo yanayolihusu taifa letu katika kuendeleza fasihi andishi kwani kama jamii itajijengea utamaduni wa kupenda kujisomea maendeleo makubwa yataonekana ndani ya fasisi andishi.

Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Cuthbert kimambo amewataka wanataaluma walioshiriki katika kongamano hilo kutumia taaluma watakayoipata kusaidia vizazi vya sasa na vya baadaye katika kutambua mambo yaliyowahi kutokea katika ukanda wa afrika na jinsi yalivyoweza kuathiri maisha ya watu ili waweze kuweka mikakati ya mahusianao ya kitamaduni na kifasihi na kuepusha majanga yaliyowahi kutokea ili kujenga maisha bora katika jamii yetu.

Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa masuala ya Utamaduni unaofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Ukumbi wa Nkrumah wakifuatilia hotuba toka kwa mgeni rasmi pamoja na Viongozi wengine wa Chuoni hapo wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa siku tatu unaohusu kujadili mambo ya utamaduni baina ya nchi za Afrika Mashariki.

Naye Mkuu wa Idara ya Lugha, fasihi ya Kingereza Dr. Eliah Mwaifuge amesema kuwa ujumbe wa kongamano hili umekua ukiendelea kuwafikia wadau wengi wa fasihi duniani kote jambo ambalo limewezesha wataalamu wengi wa fasihi kutoka nchi mbalimbali duniani kuudhuria kongamano hili la tatu hivyo kuamini yakuwa mada zinazolenga kuleta amani na kuepeka vita zitawafikia wadau mbalimbali nchi zote duniani.

Kongamaono la Utamaduni na Fasihi la Afrika Mashariki ni kongamano latatu kufanyika tokea lilipoanzishwa mwaka 2013 linalohusu taaluma za fasihi na tamaduni za afrika mashariki, ambalo limejumuhisha wadau kutoka Afrika ya Mashariki, Afrika ya Kusini afrika ya Magharibi na wadau wengine kutoka nchi za nje na kukutanisha watafiti na wanataaluma wanaoshughulika na masuala ya fasihi na utamaduni kujadili na kuchambua masuala yanayohusu amani na vita katika Bara la Afrika.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole-Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa siku tatu unaohusu kujadili mambo ya Utamaduni baina ya nchi za Afrika Mashariki unaofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi