Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

PPRA Yataja Mafanikio Kupitia Mfumo Mpya wa NeST
Nov 04, 2024
PPRA Yataja Mafanikio Kupitia Mfumo Mpya wa NeST
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, Bw. Dennis Simba akizungumza wakati akifungua mkutano wa Wahariri wa vyombo vya habari ulioandaliwa na Mamlaka hiyo kwa ajili ya kuelezea kazi na mafanikio ya mamlaka hiyo. Mkutano huo umefanyika leo Novemba 04, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Na Grace Semfuko - MAELEZO

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 iliweza kuokoa zaidi ya shilingi Bilioni 14.94 kupitia ukaguzi, na shilingi Trilioni 2.7 kupitia ufuatiliaji kwa njia ya mfumo mpya wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST), ambao umeongeza uwazi, uwajibikaji na kupunguza mianya ya rushwa.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini leo Novemba 04, 2024, Mkurugenzi wa mamlaka hiyo Bw. Dennis Simba amesema mfumo huo pia umeongeza usalama na upatikanaji wa taarifa, pamoja na kuweka mazingira mazuri na wezeshi katika mnyororo wa ununuzi wa umma.  

"Wote tunaona, katika kipindi kifupi kasi kubwa ya serikali yetu ya kujenga miradi ya maendeleo, tunaweza kuwa ni Taifa linaloongoza kwa Afrika Mashariki katika ujenzi wa miradi, hii ni kwa sababu ya umakini wa serikali yetu, miradi inatekelezeka, tuna reli ya SGR, shirika letu la ndege, miradi ya miundombinu na teknolojia, yote hayo tunayaendesha kwa umakini kupitia ukaguzi ambapo PPRA tumefanikiwa kuokoa zaidi ya Bilioni 14.94 kupitia ukaguzi, na shilingi Trilioni 2.7 kupitia ufuatiliaji kwa njia ya mfumo mpya wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST)” amesema Bw. Simba.

Ameyataja mafanikio mengine yatokanayo na ujenzi wa mfumo wa NeST kuwa ni pamoja na kusajiliwa kwa wazabuni 28,590 katika mfumo huo, kutolewa kwa mikataba ya zabuni 62,267 yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 10.2, kuwekwa kwa bajeti ya ununuzi ya zaidi ya shilingi trilioni 38.6 kwenye mfumo huo kama fursa ya wazi kwa ajili ya wazambuni pamoja na kusajiliwa kwa zaidi ya taasisi 21, 851 kwenye mfumo huo.

Aidha amezungumzia pia mgawanyo wa zabuni kwa wazawa na wazabuni wa nje ambapo mpaka kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2023/24, watanzania wamepata asilimia 99.6 ya zabuni huku China ikishika nafasi ya pili ikifuatiwa na Kenya, Afrika Kusini pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mfumo huo mpya wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST), ulianza kutumika Julai 1, 2023 ambapo umekuwa na mafanikio makubwa yakiwepo ya kudhibiti matumizi mabaya ya ofisi, kudhibiti upotevu wa fedha za umma pamoja na kukabiliana na vitembo vya rushwa katika maeneo mbalimbali.

Nae Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Bw. Deodatus Balile ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari kufungua akaunti ya mfumo wa NeST ili kuweza kupata matangazo.

“Tuwapongeze kwa kurahisisha mfumo wa ununuzi katika nchi yetu, ndugu zangu wahariri, hata matangazo ya kwenye vyombo vya habari mengi yanapitia NeST, kwa hiyo sisi tunaoendesha vyombo vya habari kama huna akaunti ya NeST huwezi kufanikisha matangazo, hali ngumu ya vyombo vya habari tuliyonayo tuna nafasi ya kujikomboa kupitia kwenye mfumo huu” amesesema Bw. Balile.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi