Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zimesaini makubaliano ya awali (MoU) ili kuongeza ushirikiano katika kupambana na rushwa kwenye ununuzi wa umma.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri na Kujenga Uwezo, Mhandisi Amini Mcharo, ikiwa siku 12 zimepita tangu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ndg. Charles Kichere alipotoa ripoti ya mwaka 2022/2023 yenye hati tisa zenye mashaka na moja chafu huku taasisi za umma sita zikipata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 390.
“Hivi ndivyo PPRA imekuwa ikitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwahudumia wananchi ili kutimiza lengo la Serikali iliyopo madarakani ya kupeleka huduma kwa wananchi na kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi na teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo,” ameeleza Mhandisi Mcharo.
Pamoja na hilo, Mhandisi Mcharo amehabarisha kuwa Mamlaka ilifanya uchunguzi kwa zabuni zilizotekelezwa katika mwaka wa fedha 2021/22 na 2022/23 na kufanikiwa kuokoa shilingi bilioni 16.27 katika jitihada za kupambana dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma, matumizi mabaya ya madaraka na viashiria vya rushwa.
“Kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 13.83 ilitokana na kuingilia kati kwa Mamlaka kwenye mikataba ambayo ilitolewa kwa wazabuni wenye bei ya juu wakati wenye bei ya chini wakitolewa kwenye mchakato na kiasi cha Shilingi bilioni 2.44 ni kiasi kilichorudishwa na wasambazaji wa bidhaa na wakandarasi kwa malipo ya ziada yaliyofanywa na taasisi nunuzi,” amearifu Mhandisi Mcharo.
Tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiendeleza kwa weledi mkubwa miradi ya maendeleo huku akipambana dhidi ya uzembe, rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa fedha za umma, na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya wateule wasio waadilifu.