Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Polisi Tabora Yamsaka Aliyetuma Meseji ya Uongo Kuhusu Kutekwa Watoto
Nov 15, 2018
Na Msemaji Mkuu

NA Tiganya Vincent

Jeshi la Polisi Wilaya ya Tabora linaendelea kumtafuta mtu aliyesambaza ujumbe wa uongo juu ya kutekwa wa wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi ChemChem uliosababisha taharuki kwa wananchi na kupelekea kuharibu mali za Polisi.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Tabora (OCD) John Mfinanga wakati akitoa ufafanuzi kwa Madiwani wa Manispaa ya Tabora kwenye kikao cha robo ya kwanza.

Alisema ujumbe huo ulisababisha kuwepo na uvunjifu wa amani ambao ulitokana na baadhi ya raia kuanza kuwashambulia Polisi na magari yao na kupelekea kupasuliwa vyoo.

Mfinanga alisema hadi leo ikiwa saa 30 zimeshapita hakuna mzazi aliyejitokeza kutoa taarifa juu ya kupotelewa na mtoto jambo linaonekana lilikuwa na uongo na lenye nia ya kuleta vurugu katika jamii.

“Waheshimiwa Madiwani ni mzazi gani anaweza kukaa zaidi ya masaa 24 mtoto wake amepotea hatoi taarifa…tunamtafuta aliyesambaza meseji hiyo ili hatimaye tumfikishe anapostahili kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria” alisema.

Aliwataka Madiwani kusaidia kuwaelimisha wapiga kura wao wanapotoa taarifa ziwe za kweli ili zisisababishe taharuki na fujo katika jambo.

Katika hatua nyingine Kamanda huyo wa Wilaya ya Tabora alisema Jeshi la Akiba Mgambo lipo kisheria na liko kwa ajili ya kusaidia majeshi mbalimbali yanapokuwa na uhitaji katika kutekeleza majukumu yao.

Alisema kama kuna miongoni mwao ambao sio waaminifu na wamekuwa wakiwaibia na kuwatesa wananchi ni vema wakatoa taarifa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao kama waarifu.

Mfinanga alisema uamuzi wa kulitumia Jeshi hilo la Akiba ulipitishwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa lengo la kusaidia katika kukabiliana na vitendo vya uharifu katika maeneo mbalimbali na sio kwa lengo la kuwaumiza wananchi.

Awali baadhi ya Madiwani wa Manispaa ya Tabora walimtaka OCD kuachana na matumizi ya Mgambo hao kwa sababu ya baadhi yao kuwa wezi, vibaka na wanaoendesha vitendo vya unyanyasaji wa wananchi wanapokuwa katika Doria.

Diwani wa Kata ya Isevya Ramadhan Kapera alisema hawawataki migambo kwa sababu ni wezi na wanachafua sifa ya Jeshi la Polisi la kulinda raia na mali zao.

Alisema kama Polisi ni wachache ni vema wakawatumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Majeshi mengine katika kukabiliana na uhalifu katika Manispaa hiyo.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Kitwala Komanya alisema kuwa baada ya kupata malalamiko kwa wakazi wa Tambuka Reli juu ya vitendo viouvu vinavyofanywa na baadhi ya Mgambo amekutana nao na kuwaonya.

Alisema Serikali haitasita kumchukulia hatua Mgambo na Polisi yoyote ambaye itabainika kuvunja Sheria ikiwemo kuiba mali za wananchi

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi