Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Polisi Tabora Yamkamata Kijana kwa Kutumia Sare za JWTZ Kutapeli
May 30, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent – RS Tabora

Mkulima mmoja Kitangili mkoani Shinyanga Francis Martin Kilalo  (31) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Tabora kwa kukutwa na sare na vifaa vingine vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambavyo anatuhumiwa kuvitumia kupateli na kuwadanganya kwa kuchukua fedha kutoka kwa vijana wanaotafuta nafasi ya kujiunga na Jeshi hilo.

Taarifa hiyo imetolewa jana na Kamanda wa Polisi wa wa Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mtafungwa alipokuwa anaongea na waandishi wa habari Ofisi kwake jana juu ya hatua mbalimbali walizochukua katika kupambana na uhalifu mkoani humo.

Alisema kuwa Polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo katika hoteli ya JM iliyopo Wilayani Igunga akiwa  na sare mbalimbali za  Jeshi la waananchi Tanzania (JWTZ) zikiwa na cheo cha Koplo ambazo ni kofia tatu, begi, sweta, buti  jozi moja, sare na  mikanda mitatu. Mali zingine zilikamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni pamoja na fomu za likizo, fomu za kujaza vijana wanaotaka kujiunga  na Jeshi hilo na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) kwa mujibu wa Sheria na hiari na mihuli yenye nembo inayofanana na Jeshi hilo.

Kamanda Mtafungwa alisema kuwa mtuhumiwa alikuwa akitumia nyaraka  na sare za Jeshi hilo kuchukua fedha kwa kuwadanganya na kuwatapeli wananchi mbalimbali kwa kudai atawatafutia ajira katika majeshi ya Kujenga Taifa na la Wananchi.

Kamanda huyo wa Mkoa wa Tabora aliongeza kuwa mtuhimiwa huyo pia alikutwa barua kutoka Serikali za mitaa za Dar es salaam na gari aina ya Toyota Starlet yenye namba za Usajili T 633 ARF ambalo wanaendelea kuchunguza uhalali wa umiliki wake na ambalo mtuhumiwa alikuwa akilitumia na kuwafanya baadhi ya wananchi wamuamini kuwa atawasaidia kupata nafasi katika majeshi.

Aliongeza kuwa mtuhimiwa huyo pia alikuwa na barua za maombi ya watu ya kuomba kujiunga na Jeshi, Fomu za Matibabu za Hospitali ya Jeshi ya Lugalo na nakala ya Vyeti vya kumaliza elimu ya Sekondari vya baadhi ya watu.

Kufuatia tukio hilo Kamanda Mtafungwa alitoa wito kwa waananchi waliowahi kutapeli ndani na nje ya Mkoa wa Tabora kujitokeza katika vituo vya Polisi ili waweze kutoa ushahidi utakasaidia kuonesha ni jinsi gani walivyumizwa na mtuhumiwa huyo.

Alisema kuwa Polisi inaendelea kushirikiana na JWTZ ili iweze kubaini sare  na vifaa hivyo alivipata wapi, kwa lengo lipi na ni nani aliyompatia ili wahusika wote waweze kufikishwa katika vyombo vya Sheria kwa hatua zaidi.

Aidha, Kamanda huyo aliwaasa wananchi kuwa makini na matapeli wanaochukua fedha na kuwadanganya kuwa watawatafutia kazi katika Majeshi kwani vyombo hivyo vinaotaratibu wake ambao ndio unaotumika kuwapata vijana wanaojiunga kwa mujibu wa sheria na wale wa hiari na sio kwa kuchangishwa fedha.

Wakati huo huo Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limefanikiwa kukamata watuhimiwa 17 kwa kukutwa na lita 205 za gongo katika msako wa kukamata wa watumiaji na wauzaji wa bidhaa hizo haramu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora Mtafungwa alisema kuwa watuhimiwa watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zao wakati wowote.

Aidha, alisema kuwa katika zoezi hilo pia Polisi ilifanikiwa kuteketeza ekari tano na nusu za mashamba ya zikiwa na uzito wa kilogramu 220 yalikuwa yamelimwa katika Msitu wa Hifadhi wa Igombe wilayani Uyui.

Alisema kuwa jitihada za kuwasaka watuhumiwa wa mashamba hayo zinaendelea na kuwaomba wananchi wenye taarifa ya walipo wahusika walisaidie Jeshi la Polisi ili wahusika waweze kufikishwa Mahakama kujibu tuhuma zao

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi