Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Pinda Awasihi Butiama Kukipokea MJNUAT
Oct 12, 2023
Pinda Awasihi Butiama Kukipokea MJNUAT
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT), Waziri Mkuu Mtaafu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa chuo hicho wakati wa ziara yake ya kutembelea chuo hicho kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo hicho Oktoba, 2022.
Na Mwandishi Wetu, MJNUAT

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT), Waziri Mkuu Mtaafu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda amewasihi wakazi wa Butiama kukipokea Chuo hicho kwa mikono miwili.

Ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa ziara  yake ya kutembelea chuo hicho kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo hicho Oktoba, 2022.

“Naomba niwasihi wakazi wa Butiama, mahusiano yetu sasa yajengwe kwa misingi ya urafiki ili mtoto huyu (chuo) aweze kuzaliwa na afya nzuri, isije ikatokea baada ya siku chache tangu kuanza kwa Chuo, matukio ya wizi yakatokea, ukisikia watu wanapanga matukio ya wizi  utoe taarifa”, alisisitiza Pinda

Alisema ujio wa Chuo hicho utapeleka mabadiliko makubwa kwa jamii inayokizunguka kutokana na kutarajia kudahili wanafunzi 6,000 ambao watahitaji huduma za kijamii kutoka kwenye jamii ya Butiama na hivyo kutoa fursa mbalimbambali za kiuchumi.

“Kwa hiyo, wale vijana wajanja wenye maono muanze kuona wanafunzi 6,000 wapo Butiama, msije mkafikia hatua ya kujilaumu kwa nini nilichelewa au kwa nini sikuliona hili", alisema Pinda

Muanzishe migahawa na huduma mbalimbali baada ya kujua wanafunzi wanataka nini, kubwa ni kwamba, nataka niwatahadharishe muweze kuliona hili msije kujilaumu,” alifafanua.

Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Mhe. Balozi Philemon Luhanjo alisema kuwa Chuo hicho kimeshindwa kufanya udahili wa wanafunzi kwa kipindi cha miaka saba kutokana na kukosekana kwa miundombinu stahiki.

“Msisitizo mkubwa umeelekezwa katika kujenga miundombinu kwa kuanza na ukarabati wa majengo yaliyokuwa Shuke ya Sekondari ya wavulana ya Oswald Mang’ombe ili yatumike.

“Nipende kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha na rasilimali watu kwa ajili ya ukarabati wa Kampasi anzilishi ya Oswald Mang’ombe, ujenzi wa Kampasi Kuu na ujenzi wa Kampasi ya Tabora utaanza hivi karibuni,” alisema  Luhanjo.  

Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kinatekeleza mradi wa ukarabati katika Kampasi yake ya Oswald Mang’ombe wenye thamani ya shilingi bilioni 2.661 na Mradi wa Elimu ya Juu Kwa Mageuzi ya Kiuchumi katika Kampasi Kuu Butiama na Kampasi ya Tabora wenye thamani ya shilingi bilioni 102.5

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi