Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Pato la Mtanzania Laongezeka kwa Asilimia 11.
Jun 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_2941" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017/2018 Bungeni Mjini Dodoma.[/caption]

Na Raymond Mushumbusi.

Pato la kila Mtanzania kwa mwaka 2016 limeongezeka kwa asilimia 11 kutoka shillingi 1,918,897 kwa mwaka 2015 mpaka kufikia shillingi 2,131,299 kwa mwaka 2016.

Takwimu hizo zimebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango  Dkt. Philip Mpango wakati akiwasilisha Bungeni Mjini Dodoma taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2016 na mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017/2018.

Akifafanua kuhusu ongezeko hilo Dkt. Philip Mpango amesema kuwa Pato la Taifa kwa mwaka 2016 lilifikia Shillingi million 103,744,606 kwa bei za mwaka husika na kiasi hiki kiligawanywa kwa idadi ya watu 48,676,698 waliopo Tanzania Bara na kufanya wastani wa Pato la kila Mtanzania kufikia kiasi cha Shillingi 2,131,299.

Ameeleza kuwa kwa thamani ya Dola za Marekani, wastani wa pato la Kila mtu liliongezeka kutoka Dola 967.5 mwaka 2015 hadi Dola 979.1 kwa mwaka 2016 ikionesha kuwa Tanzania inaelekea kwenye kundi la Uchumi wa kati.

“Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali ili tuweze kufikia uchumi wa kati kwa kuongeza fursa mbalimbali za uzalishaji nchini” alisisitiza Mhe. Dkt Mpango.

Dkt. Philip Mpango ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuboresha shughuli za uzalishaji wa tija katika sekta zinazoajiri hususan katika sekta ya kilimo cha mazao,ufugaji na uvuvi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi