Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Nidhamu Awamu ya Tano Yaongeza Kasi ya Utekelezaji Miradi
Jan 08, 2018
Na Msemaji Mkuu

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Na. Fatma Salum

Nidhamu katika ukusanyaji na matumizi ya fedha za umma na dhamira ya dhati ya kutekeleza ahadi kwa faida ya wananchi, vimesaidia Serikali ya Awamu ya Tano kuendelea kutekeleza kwa mafanikio miradi mikubwa ya kitaifa.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi (katikati aliyenyoosha mkono) akiongea na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania na utekelezaji wa miradi mbalimbali. Kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi anayehusika na Usajili, Patrick Kipangula na kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Habari na Picha, Rodney Thadeus.

Dkt. Abbasi alisema kuwa hali ya uchumi wa nchi inaendelea kuimarika kwa kiasi cha kuziridhisha taasisi mbalimbali za kimataifa zikiwemo Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB).

“Ripoti za Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Taasisi ya Goldman Sachs ya Marekani zimetabiri kuwa uchumi wa dunia utakua kwa wastani wa asilimia 3.0 hadi 4.0, ambapo ukuaji wa uchumi wa Tanzania unatajwa kuendelea kuwa kati ya nchi tano bora za Afrika ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7.0 katika mwaka 2018”, alifafanua Dkt. Abbasi.

Kiwanda cha SAYONA Mwanza

Akizungumzia kuhusu jitihada za Serikali katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, Dkt. Abbasi alisema kuwa kufikia mwaka jana viwanda zaidi ya 3,300 vilisajiliwa, kupitia Msajili wa Makampuni 250, Kituo cha Uwekezaji (361, Mamlaka ya Usimamizi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi 41 na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO lililosajili viwanda vidogo vya kati ya mtu mmoja hadi tisa vipatavyo 2,721. Ujenzi na uzalishaji katika viwanda hivi uko katika hatua mbalimbali.

Kati ya miradi hiyo iliyosajiliwa, viwanda vikubwa ni 652 vyenye jumla ya mtaji wa zaidi ya TZS trilioni tano utakaowekezwa nchini na vitaajiri watu 50,625.

Kiwanda kidogo cha Kusindika Vitungu Saumu kilichopo Wilaya ya Mbulu mkoa wa Manyara

Kuhusu miradi mikubwa ya umeme Dkt. Abbas alibainisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi zaidi ya 20 ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika. Miongoni mwa miradi hiyo ni usimikaji wa mitambo ya umeme wa gesi Kinyerezi I ambao utaongeza Megawati 185 na Kinyerezi II Megawati 240. Mitambo hii kwa pamoja itaongeza megawati 425.

“Mtambo wa Kinyerezi I-Nyongeza umefikia asilimia 50 na mtambo wa Kinyerezi II umekamilika kwa asilimia 87 ambapo Desemba, 2017 umeingiza megawati 55.94 katika Gridi ya Taifa. Kiasi kingine cha megawati 27.94 kinatarajiwa kuingia kwenye gridi mwezi huu wa Januari na mitambo yote miwili itakamilika mwaka huu,” alisema Dkt. Abbas.

 

Mradi wa Umeme wa Kinyerezi II

Aidha, Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) kwa kuanzia na kipande cha kilometa 300 (Dar-Moro) kitakachogharimu TZS trilioni 2.7 wakati huo huo ujenzi wa kipande cha pili cha kilometa 442 (Morogoro-Makutupora, Dodoma) kitakachogharimu TZS trilioni 4.3, mkandarasi ameshaanza maandalizi.

Wakati ujenzi wa reli ukiendelea, Dkt. Abbas alisema Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) imeshatangaza zabuni kwa ajili ya kupata makampuni yatakayotengeneza vichwa na mabehewa ya kisasa ya treni ya umeme na mafuta.

Moja ya mfano wa Treni zinazotumia umeme. Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) imetangaza zabuni ya ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa kwa ajili ya kutumika katika Reli mpya ya kisasa (SGR)

Katika zabuni hiyo Serikali inatarajia kununua vichwa 25 (23 vya umeme na 2 vya dizeli), mitambo 25 ya ukarabati wa reli na mabehewa 1,590 (kati ya hayo 1,530 yakiwa ni ya aina mbalimbali za mizigo kama vile kubeba makontena, nafaka, mafuta n.k), mabehewa 60 ni ya abiria (15 yakiwa ni daraja la kwanza na 45 daraja la kawaida).

“Kwa upande mwingine Serikali imefanikiwa kukamilisha mradi wa meli mbili mpya za mizigo za MV Njombe na MV Ruvuma zinazobeba mizigo tani 1,000 na tayari zimeanza safari kwenda bandari mbalimbali zikiwemo za nchi jirani,” alifafanua.

Vilevile katika Ziwa Victoria tayari meli ya abiria ya MV Clarios na ya mizigo MV Umoja zilizofanyiwa ukarabati na kuwa za kisasa zimeshaanza kazi.

Akielezea kuhusu Tasnia ya habari, Dkt. Abbasi alitoa rai kwa Waandishi wa Habari ambao kwa mujibu wa Sheria mpya ya Habari hawana elimu kuanzia ngazi ya Stashahada kwenda kujiendeleza kitaaluma kabla muda uliotolewa haujaisha.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi