Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja amewataka washiriki wa Mkutano wa nchi zinazotekeleza Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimaji Wadogo wa Dhahabu kuja na mikakati ya pamoja itakayosaidia kuondokana na matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa madini hayo.
Ameyasema hayo, leo Novemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa nchi za Afrika zinazotekeleza mradi huo.
"Lengo ni kuondokana na matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu kufikia 2030, matumizi ya zebaki yana athari kubwa kwa binadamu na mazingira kwa ujumla wake", amesema Mhandisi Luhemeja.
Akieleza kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania amesema kuwa, ni pamoja kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki za uchenjuaji dhahabu kwa wachimbaji wadogo.
Amezitaja nchi zinazotekeleza mradi huo kuwa ni Ghana, Senegal, Kenya, Zambia na Tanzania ambako kuna wachimbaji wadogo wa dhahabu ambao wanatumia zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu.
" Serikali inaendelea na jitihada za kuelimisha wananchi hasa wachimbaji wadogo wa dhahabu kuhusu athari za matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu, tunaishukuru Benki ya Dunia na Mfuko wa Mazingira Duniani kwa kuwezesha mkutano huu kufanyika kwa mafanikio hapa Tanzania." amesema Luhemeja.
Akieleza hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali Mhandisi Luhemeja amesema kuwa ni pamoja kutekeleza Mkataba wa Minamata unaotaka jitihada za pamoja katika mapambano dhidi ya matumizi ya zebaki.
Kwa upande wake mwakilishi wa Benki ya Dunia Bw. Makiko Watabane amesema mkutano huo ni matokeo ya jitihada za kupambana na matumizi ya zebaki na uchafuzi wa mazingira ambavyo ni vyanzo vya vifo.
"Kila mmoja katika jamii yetu anaguswa na madhara ya matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu na uchafuzi wa mazingira", alieleza Watabane.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema ushirikiano wa nchi zinazotekeleza mradi huu kwa pamoja utasaidia kukabili changamoto ya matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu.
Amebainisha kuwa zebaki ina madhara makubwa katika mazingira na binadamu.
Mkutano wa nchi za Afrika zinazotekeleza Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu (EHPMP) unalenga kuja na mikakati ya pamoja yakuondokana na changamoto ya madhara ya zebaki katika mazingira.