Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC zinatakiwa kukuza uelewa wa shughuli za SADC kwa wananchi
Oct 02, 2018
Na Msemaji Mkuu

 Zamaradi Kawawa, MAELEZO, Windhoek, Namibia

29 Septemba 2018

Nchi  wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC zinatakiwa kukuza uelewa wa shughuli za SADC kwa wananchi wake kwa  kufundisha mashuleni historia ya ukombozi wa    nchi hizo pamoja na kutumia  wimbo wa SADC na bendera yake kwenye shughuli za kitaifa na kimataifa.

Baraza la SADC la Mawaziri wa nchi wanachama wanaoshughulikia sekta za Mawasiliano, Habari, Ujenzi na Uchukuzi walikubaliana hayo katika kikao kilichofanyika  Septemba 27,2018 Windhoek, Namibia baada ya kufunguliwa na Waziri wa Madini na Nishati  wa Namibia Mheshimiwa Tom Alweendo kwa niaba ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo.

Kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC kilisema wananchi wa SADC wanatakiwa  kuelimishwa  kuhusu SADC kwa kufahamu historia yake na ukombozi  wa nchi wanachama,  alama za SADC zikiwemo bendera, nembo, wimbo na itifaki yake kwa kuhusisha elimu hiyo kwenye mtaala wa elimu kwa nchi wanachama.

Akifungua kikao hicho,  Waziri wa Madini na Nishati wa Namibia Mheshimiwa Alweendo alisema kuna taarifa nyingi nzuri za kuwaeleza wananchi wa nchi wanachama kuhusu SADC hivyo ni jukumu la Serikali za nchi za SADC kuelimisha na kuwaeleza wananchi wake wakati chombo hicho kkiendelea kujiimarisha.

Kikao hicho cha siku moja  kilichokutana kwa lengo la kupitia utekelezaji wa  mipango  ya maendeleo ya nchi wanachama kwenye maeneo ya sekta za Mawasiliano, Habari, Ujenzi na uchukuzi  kilisimama kwa dakika moja kabla ya kuanza ili  kuonyesha masikitiko yao kwa  vifo vya watanzania zaidi ya 200 vilivyotokana na ajali ya MV Nyerere Ziwa Victoria, Mwanza.

Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo bi. Susan Mlawi kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ambaye kwa niaba ya Serikali alipokea salamu za pole kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo kufuatia vifo vya watanzania zaidi ya 200 vilivyotokana na ajali ya MV Nyerere kwenye Ziwa Victoria mkoani Mwanza hivi karibuni.

Aidha, Kikao hicho kiliipongeza Tanzania kwa kupata tuzo ya dunia ya usalama wa anga baada ya kufaulu kwa kukidhi vigezo vilivyowekwa na Baraza la usafiri wa anga duniani vinavyohusu uhakika wa usalama wa anga.

Wakati wa kikao hicho cha baraza la SADC la Mawaziri  wa sekta za Mawasiliano, Habari, Ujenzi na Uchukuzi, Bi Mlawi alieleza nia ya Tanzania ya kupeleka  mgombea kwenye nafasi ya Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na kuomba ushirikiano wa  nchi wanachama wa SADC  wakati wa uchaguzi ukifika.

Alimtaja mgombea huyo kuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dr Agnes Kijazi, mwanamke msomi wa ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) mwenye uzoefu wa miaka 30 kwenye masuala ya hali ya hewa kutoka nchi za SADC.

Mheshimiwa Alweendo kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho alisema nchi wanachama wa SADC zimepiga hatua kubwa kwenye masuala ya hali ya hewa kwa kutumia  teknolojia ya kisasa ya satellite iliyoimarisha kwa kiasi kikubwa matokeo ya utabiri wa hali ya hewa hivyo kuwezesha  nchi kukabiliana na majanga ya ukame, mafuriko na moto yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dr. Agnes Kijazi ambaye pia alitambulishwa katika kiako hicho aliiambia Idara ya Habari-MAELEZO kuwa  Tanzania inajipanga kutekeleza miradi miwili mikubwa ya SADC ikiwemo uboreshaji wa  chuo cha yaifa cha hali ya hewa kilichopo Kigoma pamoja na  uwekaji wa miundo mbinu ya kisasa ya utabiri wa hali ya hewa  itakayoimarisha huduma za utabiri wa hali ya hewa kwa nchi ili kupunguza umaskini.

Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC ina nchi wanachama 16 zikiwemo Namibia ambaye ni mwenyekiti na Tanzania ni Makamu mwenyekiti wa Jumuiya hiyo. Nchi nyingine ni Zimbabwe, Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Botswana, Angola, Msumbiji, Eswati, Lesotho, DRC, Mauritius, Comoro, Seychelles na Moroco.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi