Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

NCAA Yazindua Mfumo wa Utalii Mtandao Kuwaunganisha Wadau Duniani.
Apr 22, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi wetu - NCAA

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imezindua mfumo mpya wa Utalii Mtandao “Tourism Web Camera” unaolenga kuwaleta pamoja watu mbalimbali Duniani kuona vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid19 ambapo wageni wengi wamefungiwa katika nchi zao.

Uzinduzi wa mfumo huo uliohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda umelenga kuunganisha watu mbalimbali ulimwenguni kuweza kufuatilia vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo ambapo kwa kuanzia watazamaji wataona vivutio hivyo bure na baadae kuchangia kiasi kidogo cha pesa katika kuendeleza uhifadhi  wa rasilimali na vivutio katika hifadhi hiyo.

Prof. Mkenda ameelezea kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na NCAA katika kuwafikia wadau wake pamoja na kukabiliana na changamoto za ukosefu wa wageni kutokana na janga la Korona.

Amebainisha kuwa shughuli za ulinzi na uhifadhi wa rasilimali ndani ya hifadhi ni suala endelevu na lazima kuendelea kuwahabarisha wageni kuhusu yanayojiri ndani ya Hifadhi hiyo hasa kipindi hiki ambacho wengi wamezuiliwa kusafiri.

“Tunajua kuwa kwa sasa watalii wengi nchi zao ziko kwenye ‘lockdown’ na hawawezi kusafiri, NCAA mmefanya kitu chenye maana katika kutafuta namna ya kuwafikia huko huko walipo na kuendelea kufurahia utalii wa Ngorongoro popote Duniani, ni imani yangu kuwa hatua hii itasaidia kuwa andaa watu kisaikolojia wasisahau kuhusu vivutio vya Ngorongoro hata baada ya janga hili kupita”, ameongeza Prof. Mkenda.

Prof Mkenda ameongeza kuwa mtazamo wa Rais Dkt John Pombe Magufuli ni kuhakikisha kuwa tunaendelea kujilinda na kujipanga huku tukihakikisha kuwa baada ya janga la Corona kupita uchumi wa nchi yetu unarudi kama ulivyokuwa.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Freddy Manongi amebainisha kuwa mfumo huo wa utalii mtandao kwa njia ya “Live streaming web camera” uliozinduliwa unalenga kuwafikia watu mbalimbali duniani kuona bure kwa kufungua Youtube channel na kuandika neno Ngororongoro Conservation Areakwa ajili ya kufuatilia vivutio katika hifadhi hiyo.

“Tumeshuhudia anguko katika sekta ya Utalii baada ya janga la Covid 19 ambapo kwa sasa inapita siku nzima bila kupata mgeni hata mmoja, kwa hiyo tumeamua kubuni teknolojia hii ya kuwaleta pamoja wateja wetu duniani kote ambao kupitia mfumo huu wataona vivutio vya Ngorongoro Mubashara wakiwa majumbani mwao”

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa NCAA anayesimamia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Bw. Jocktan Bikombo amebainisha kuwa mfumo huo wa ‘live streaming’ umeunganishwa na Camera mbalimbali zilizofungwa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ili kuhakikisha kuwa wateja wetu wanapata ladha tofauti ya vivutio vilivyopo.

Uzinduzi wa mfumo huo umeenda sambamba na majaribio ya kuunganisha moja kwa moja wadau mbalimbali waliopo Paris nchini Ufaransa na London Nchini Uingereza ambao wamethibitisha kuuona na kushuhudia vivutio hivyo kwa njia ya mtandao.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi