Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Nawaomba Watanzania Tushirikiane katika Mambo Makubwa ya Msingi: Rais Magufuli
Nov 02, 2018
Na Msemaji Mkuu

 

Na. Immaculate Makilika

Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewa himiza watanzania kushirikiana na Serikali yake katika masuala makubwa ya msingi ili kuliletea Taifa maendeleo ya haraka

Akizungumza leo katika ukumbi wa Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam,  wakati wa  Kongamano kuhusu hali ya uchumi na Siasa nchini, lenye mada isemayo “Miaka Mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano Tunatoka Wapi, Tuko Wapi na Tunakwenda Wapi?”, Rais Magufuli alisema kuwa anawaomba watanzania kuendelea kushirikiana Serikali yake ili kujiletea maendeleoa.

“Nawaomba watanzania katika mambo makubwa ya msingi ni lazima tusimame kwa pamoja, na si kujali itikadi za vyama vyetu vya siasa”alisema Rais Magufuli

Aidha, alisisitiza kuwa “ mambo ya chama yatatuchelewesha, watanzania hawataki vyama, wanataka maendeleo”

Katika kongamano hilo ambalo Rais Magufuli alikuwa mgeni maalum, amesisitiza namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwaletea maendeleo watanzania kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kujenga uchumi.

Rais Magufuli amekaribisha sekta binafsi katika kilimo ili kuimarisha sekta hiyo kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa na ikiwa ni pamoja na kupata soko la uhakika la mazao ya wakulima.

“Benki ya kilimo ina shilingi bilioni 300, sekta binafsi wanaweza kuja kushirikiana na Serikali kwa kuanzisha viwanda vitakavyosaidia sekta hiyo ya kilimo” alisema Rais Magufuli

Kuhusu matumizi ya lugha ya kiswahili, Rais Magufuli alisema aliamua kuzungumza kiswahili kwa sababu kiswahili ni utamaduni wa mtanzania, lakini ni lugha ya kumi kwa kuwa na wazungumzaji wengi duniani, na ni lugha ya pili Afrika.

Hivyo, amewataka watanzania kukithamini zaidi kiswahili, licha ya kuwa wanaweza kujifunza lugha nyingine zozote.

Sambamba na hilo, Rais Magufuli ambaye amezungumza baada ya kusikiliza mada tano zilizotolewa na wanataaluma wakongwe wa uchumi, lugha, siasa na utawala amnbapo Rais aliahidi kufanyia kazi mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa katika kongamano hilo, ambayo anaamini yataleta tija na maendeleo kwa Taifa.

Mada zilizowasilishwa na kujadiliwa ziligusia masuala mbalimbali kama vile viwanda, nishati ambapo ifikapo mwaka 2020 vyanzo vya nishati jadilifu na visivyojadilifu vitazalisha megawati  5,000 na mwaka 2025 megawati 10,000 za umeme.

Aidha, mafanikio mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na ukuaji wa uchumi kwa asilimia saba na jitihada sahihi zinazofanywa kuelekea asilimia nane, na kufanya Tanzania kuongoza katika nchi za Afrika Mashariki, na kuwa  miongoni mwa nchi 5 za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Vile vile, katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano, pamoja na mafanikio mengine makubwa ya kufufua miradi ya msingi wezeshi, kama ununuzi wa ndege saba, uboreshaji wa bandari, viwanja vya ndege na barabara ni fursa ya kuwezesha miaradi mingine ya kiuchumi,mfano,viwanda vipya zaidi ya 3,066, vilivyojengwa vitahitaji huduma za maji umeme, barabara, bandari kama mahitaji wezeshi ya msingi.

Huduma kama usafiri wa anga zimeboreshwa, ikiwemo sekta ya utalii ambapo mikakati ya sekta hiyo, matarajio yake mwaka ujao watalii wanaotarajiwa kutembelea Tanzania wataongezeka hadi kufikia milioni 2, kiwango kitakachokuwa karibu mara mbili ya watalii waliokuwa wanatembelea Tanzania miaka ya nyuma

Katika kongamano hilo, wahudhuriaji walipata fursa ya kujadili  mada zilizotolewa, ambazo kwa ujumla tafiti za mada zimebaini juhudi kubwa alizofikia Rais na Serikali yake kwa muda mfupi na wasomi tafiti zao zimebaini kuwa  miradi mikubwa inayoendelea vema, itawezesha miradi mingine kuanzishwa au kufufuliwa na kuleta maendeleo, mfano ujenzi wa Umeme ni mradi utakaowezesha ujenzi wa viwanda, pia wameeleza changamoto na kutoa maoni.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na watendaji mbambali  wa Serikali, wakiwemo viongozi wastaafu, wabunge pamoja na wanafunzi wa vyuo na sekondari.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi