Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ametembelea na kukagua hali ya utoaji wa huduma katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI
Jun 24, 2020
Na Msemaji Mkuu

 Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

24/06/2020 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel ametembelea na kukagua hali ya utaoaji wa huduma katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI pamoja na kuzumza na watumishi ili kufahamu changamaoto mbalimbali wanazozipata katika kutekeleza majukumu yao ya kazi za  kila siku.

Akizungumza na viongozi wa Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam Dkt. Mollel alisema  Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli imefanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya hususani katika  kuimarisha  huduma za kibingwa hapa nchini.

“Kuwepo kwa uwekezaji huu kumewafanya wataalamu wa Taasisi ya MOI kuokoa maisha ya watanzania wengi ambao wametibiwa hapa nchini pia imeokoa zaidi ya bilioni 38.4 ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa hao kufuata huduma za kibingwa nje ya nchi. Haya ni mafanikio makubwa ambayo lazima watanzania wafahamu kwamba  Serikali hii inawajali wananchi wake,” alisema Dkt. Mollel.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface alisema  katika Uongozi wa Serikali ya awamu ya tano Taasisi hiyo ilipokea bilioni 16.5 kutoka Serikalini fedha ambazo zilitumika kukamilisha mradi wa ujenzi wa awamu ya tatu ya MOI pamoja na kununua vifaa tiba vya kisasa ambavyo vimesaidia kupatikana kwa  huduma nyingi za kibingwa na hivyo kumaliza rufaa za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.

“Tumeanzisha huduma nyingi za kibingwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye Taasisi yetu, wiki iliyopita Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alizindua kituo cha kitaifa cha teleradiolojia kilichopo hapa MOI na wiki chache zijazo tutaanza majaribio ya mitambo ya maabara ya upasuaji wa Ubongo,” alisema Dkt. Boniface.

Dkt. Boniface alisema huduma ya maabara ya upasuaji wa Ubongo bila kufungua fuvu itaanza kutolewa hapa nchini wiki chache zijazo na hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazotoa huduma hiyo.

“Uwepo wa Maabara hii utatupa heshima kama nchi kwani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati hakuna maabara yenye vifaa vya kisasa kama hivi ambavyo Serikali ya awamu ya tano imevinunua na kusimikwa hapa MOI, kwa hili tunamshukuru sana Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli,” alishukuru Dkt. Boniface.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa hospitali za Umma na binafsi kutoka Wizara ya  Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Vivian Wonanji alisema  uwepo wa huduma nyingi za kibingwa hapa nchini kumetokana na mpango makakati wa Wizara wa mwaka 2017 ambao ulijikita katika kuboresha huduma za kibingwa ili kumaliza rufaa za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Naibu Waziri Mollel akiwa katika Taasisi hiyo alitembelea vitengo vya  huduma ya dharula, radiolojia, kitengo maalum cha tiba mtandao  pamoja na kuzungumza na wagonjwa aliowakuta wanapata matibabu katika vitengo hivyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi