Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Mabula Ataka Wadau Kushirikishwa Utekelezaji Mpango Kabambe
Aug 13, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, MANYARA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinashirikisha wadau wa sekta mbalimbali wakati wa utekelezaji Mpango Kabambe katika maeneo yao.

Aidha, alitaka mipango inayoandaliwa katika Halmashauri za Miji na Majiji kuhakikisha inazingatia mipango kabambe inayoandaliwa ili kuifanya miji kuwa na taswira nzuri.

Dkt. Mabula alieleza hayo Agosti, 12 2021 wilayani Babati mkoani Manyara wakati akizindua Mpango Kabambe wa Mji wa Babati akiwa katika ziara yake ya siku moja ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika Mkoa wa Manyara.

Alisema,  ni vizuri watendaji wa  halmashauri kuhakikisha wakati wa utekelezaji mipango kabambe wanashirikisha wadau kama vile sekta za maji, barabara na umeme na kusisitiza kuwa hawatakiwi kwenda kinyume na yaliyowekwa katika mpango huo ili kuifanya miji kuwa na taswira nzuri na inayovutia.

Naibu Waziri wa Ardhi aliongeza kuwa, Wizara yake inaendelea kuhamasisha uandaaji mipango kabambe kwenye maeneo mengine nchini ili kuongeza kasi ya upimaji pamoja na kuifanya miji kuwa katika sura nzuri.

"Kikubwa utekelezaji uzingatie mpango na lazima uwekwe wazi kwa kushirikisha wadau na kumkabidhi kila mdau kipande chake cha utekelezaji mfano barabara TANROAD au TARURA akabidhiwe, umeme TANESCO na maji wapewe mamlaka ya maji na utekelezaji uzingatie mpango usiende kinyume" alisema Dkt. Mabula 

"Unakuta barabara nzuri halafu anakuja mtu wa maji anapitisha mabomba yake na anaharibu kabisa na hapa lengo ni kuona miji yote inapangwa vizuri", Naibu Waziri Mabula.

Aidha, Dkt Mabula aliuelezea mpango kabambe aliouzindua kama njia mojawapo ya kutoa fursa za ajira sambamba na kuongeza kasi ya upimaji na hivyo kupunguza ama kuondoa migogoro ya ardhi.

Alizitaka Halmashauri ambazo bado hazijandaa mipango kabambe kuiga mfano wa halmashauri ya mji wa Babati kwa kuandaa mipango kabambe ili kuchangia shughuli za kiuchumi na kuagiza ofisi za mikoa na wilaya kufuatilia na kupatiwa ripoti ya utekelezaji Mpango Kabambe katika halmashauri husika ili kuleta maendeleo ya kichumi na kimazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Imaculata Senje alisema lengo la serikali katika uandaaji mpango kabambe ni kuona kasi ya upangaji inaoongezeka.

Kwa mujibu wa Bi. Senje, hadi sasa jumla ya mipango kabambe 30 imeandaliwa kwenye makao makuu ya wilaya nchini na kusisitiza kuwa mipango hiyo inapoandaliwa hushirikisha sekta zote muhimu kama vile barabara, maji, umeme nk.

 "Mipango unapoandaliwa inazingatia miradi ya kutekelezwa inayogusa sekta zote na ndiyo maana wakati wa uandaaji tunashirikisha sekta zote na gharama zinazoainishwa katika mpango ni kwa ajili ya miaka ishirini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi