Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Kihenzile Asisitiza Kasi Mradi wa Boti Ziwa Viktoria
Dec 23, 2023
Naibu Waziri Kihenzile Asisitiza Kasi Mradi wa Boti Ziwa Viktoria
Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile akisisitiza jambo kwa Watumishi wa Serikali na Wadau (hawapo pichani) wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi wa ujenzi wa boti yenye vifaa vya matibabu (Ambulance Boat), iliyofanyika jijini Mwanza.
Na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile amelitaka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuhakikisha mradi wa ujenzi wa boti yenye vifaa vya matibabu (Ambulance Boat) unakamilika kwa wakati na viwango ili kuwawezesha wakazi wa ziwa Viktoria na visiwa vyake kuanza kutumia huduma hiyo.

 

Akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba huo baina ya TASAC na Kampuni ya LOCA, Muhendislik Gemi Mak. PLas Ve Gd. San Tic ltd Sti ya nchini Uturuki jijini Mwanza Naibu Waziri Kihenzile amesema kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi na watumiaji wa usafiri majini hususani nyakati za majanga.

 

“Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri kwa wananchi wanaotumia ziwa Viktoria na kupitia mradi huu wa boti yenye vifaa tiba kutaokoa watumiaji wa usafiri wa majini na wananchi kwa ujumla kwa kupata huduma za afya pindi inapotokea ajali katika ziwa viktoria”, amesema Naibu Waziri Kihenzile.

 

Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kuwa pamoja na utekelezaji wa mradi huo, kwa sasa Serikali iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha Utafutaji na Ukoaji ambacho kitafanya kazi kwa ushirikiano na kituo cha Dar es Salaam ili kuimarisha usalama katika usafiri majini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bi. Amina Makilagi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha usafiri huo kwa kuwekeza katika ujenzi wa meli na maboresho ya miundombinu lengo likiwa kuchagiza uchukuzi katika Ziwa Viktoria.

 

Mkuu wa Wilaya Makilagi ameongeza kuwa mradi huu umekuja wakati muafaka kwani kukamilika kwake kutachangia kuokoa maisha ya wananchi kwani watapata huduma hiyo kwa wakati.

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Nahodha Musa Mandia amemuhakikishia Naibu Waziri Kihenzile kuwa Bodi na Menejimneti zimejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na viwango.

 

Mradi wa ujenzi wa boti yenye vifaa vya matibabu unaotekelezwa na kampuni ya Kampuni ya LOCA Muhendislik Gemi Mak. PLas Ve Gd. San Tic ltd Sti ya unatarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni nne na unatarajiwa kukamilika ndani ya kumi na mbili (12).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi