Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Kasekenya Awataka Watendaji Kufanya Maamuzi
Jan 13, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ameitaka menejimenti na viongozi wa taasisi wa Sekta ya Uchukuzi kufanya maamuzi ili kutochelewesha maendeleo kwa wananchi katika utekelezaji wa miradi.

Ametoa kauli hiyo wakati akifunga mkutano wa siku mbili wa baraza la Wafanyakazi la sekta ya Uchukuzi lililofanyika mkoani Mwanza na kusema kuwa awamu hii imejikita katika matokeo na sio mazoea.

“Katika awamu hii watendaji wengi wamekuwa wakichelewa kutoa maamuzi katika maeneo mbalimbali sababu ya kutojiamini hii inafanya utekelezaji wa miradi kuchelewa kukamilika na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi” amesema Mhandisi Kasekenya.

Mhandisi Kasekenya amebainisha umuhimu wa kuwa na ratiba ya ukaguzi wa miradi kwa kila muhula na kusisitiza kuwa ukaguzi huo utawezesha kupunguza changamoto zinazojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi.

“Namna bora ya kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye miradi ni kuwa na ratiba ya kukagua miradi hiyo mara kwa mara, na ratiba hizo zipangwe kwa miradi yote inayotekelezwa chini ya Sekta’ Amesisitiza Mhandisi Kasekenya.

Aidha, Mhandisi Kasekenya amesema kuwa ni muhimu wataalam wa sekta walio kwenye miradi kuchukua ujuzi wakati huu ambapo miradi inaendelea ili utaalam huo uwasaidie kusiimamia vizuri miradi itakapokamilika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza na Kaimu Katibu Mkuu Gabriel Migire ameahidi kutekeleza maagizo hayo na kusisitiza kuwa kitengo cha Ufatiliaji na Tathimini-Uchukuzi kitaboresha zoezi hilo na kuhakikisha linafanyika na kuleta matokeo chanya.

Baraza la Wafanyakazi la sekta ya uchukuzi lililofanyika kwa siku mbili mkoani Mwanza limejumuisha menejementi na watumishi wa kila idara katika sekta na wakuu wa taasisi zilizo chini yake ambapo pamoja na mambo mengine limepitia utekelezaji wa miradi ya sekta na kuweka mikakati mbalimbali ya kuboresha utendaji wa sekta.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi