Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kanyasu Awaonya Wananchi Wanaotoa Vitisho kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji
Jun 03, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_43831" align="aligncenter" width="800"] Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungumza na wahitimu wakati akifunga mafunzo ya Askari 20 wa Wanyamapori wa Vijiji kutoka mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Singida waliohitimu mafunzo hayo katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kilichopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.[/caption]

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amewataka Wananchi waache tabia ya kuwatishia maisha Askari wanyamapori wa Vijiji (VGS) wakati wanapowakataza wananchi hao kuendesha shughuli za kibinadamu katika maeneo ya mtawanyiko na mapito ya wanyamapori (shoroba)

Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Mhe. Sophia Mfaume afanye uchunguzi kwa kutumia vyombo vyake vya usalama ili kuwabaini Wananchi hao wanaowatishia Askari wanapotekeleza majukumu yao na watakaobainika hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Mhe. Kanyasu, ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya Askari  20 wa  Wanyamapori wa Vijiji  wa kutoka mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Singida waliohitimu mafunzo hayo  katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kilichopo katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma

“Leo mmehitimu na tumewaapisha, mmekuwa askari kweli lakini tambueni kuwa kazi za kiuchumi zinapelekea uharibifu mkubwa sana wa mapito ya wanyama, nendeni mkawaelimishe wananchi wasiendelee kuharibu kwa ustawi wa hifadhi zetu", alisema Kanyasu.

[caption id="attachment_43832" align="aligncenter" width="800"] Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akikagua paredi kwa Askari 20 wa Wanyamapori wa Vijiji wa kutoka mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Singida wakati akifunga mafunzo kwa wahitimu wa mafunzo hayo katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kilichopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Ruvuma.[/caption]

Amefafanua kuwa maeneo ya mtawanyiko na shoroba lazima zilindwe ili kuruhusu wanyamapori waendelee kuzaliana na pia kwenda kupata virutubisho maalum ambavyo havipo mbugani.

''Tunazihitaji hizi shoroba, tulikuwa tumejisahau shoroba nyingi zimekuwa mashamba na makazi na wanyama wamekuwa hawana sehemu ya kupita, maeneo ya mtawanyiko yasipokuwepo utalii na Hifadhi vitatoweka '' amesema Kanyasu

"Lazima tufike mahali tuamue eneo hili ni kwa ajili ya kilimo na eneo hili kwa ajili ya makazi, haiwezekani maeneo yote tukaanzisha kilimo na makazi ilhali wanyamapori hawana mipaka" Alisisitiza Kanyasu.

Amesema uwepo wa shoroba na maeneo ya mtawanyiko husaidia kupata kizazi imara cha wanyamapori kwani wakifungiwa sehemu moja huzaliana ndugu na kukosa ubora,ikiwamo kuwa rahisi kushambuliwa na magonjwa.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka askari hao kufanya kazi kwa uaminifu kwa kujiepusha kuungana na mtandao wa majangili.

[caption id="attachment_43833" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya Askari wa wanyamapori wa Jamii wakiwa wanamsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu wakati akizungumza nao katika mahafali ya kufuzu mafunzo yao katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili cha Likuyu Sekamaganga.[/caption]

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Mhe. Sophia Mfaume amewahakikishia askari hao kuwa wafanye kazi kwa kufuta sheria na wale watakaowakwamisha katika kutekeleza majukumu yao hatasita kuwachukulia sheria.

Aidha, Amewataka Wananchi wafuate sheria kwa kuheshimu maeneo ya mtawanyiko na shoroba ili Hifadhi ziendelee kuwepo

Kwa upande wake, Mhitimu wa mafunzo hayo Musa Alfred Wakati akisoma risala, Amemueleza Naibu Waziri kuwa mafunzo waliyopewa yatakuwa chachu katika shughuli za uhifadhi nchini.

Naye Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Ruvuma, Jaqueline Msongozi amewataka askari hao wa vijiji watekeleze majukumu yao bila kutishwa na mtu yeyote kwa vile maliasili hizo ni za watanzania wote na wao wanazilinda kwa niaba ya Watanzania.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi