Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Muhimbili Kuanzisha Huduma ya ‘3D Printing’ kwa Wagonjwa wa Kinywa, Meno
Oct 25, 2023
Muhimbili Kuanzisha Huduma ya ‘3D Printing’ kwa Wagonjwa wa Kinywa, Meno
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi akizungumza wakati alipokutana na uongozi wa Taasisi ya MCW kwa lengo la kujadili namna ya kuhakikisha huduma hiyo inaanzishwa haraka katika Hospitali ya Upanga na Mloganzila.
Na Mwandishi Wetu

Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) kwa kushirikiana na Taasisi ya Miracle Corner World (MCW) kutoka nchini Marekani inatarajia kuanzisha huduma ya matibabu ya magonjwa ya kinywa na meno kwa kutumia teknolojia ya ‘3D printing’ ambayo inarahisisha utengenezaji wa meno bandia, vifuniko vya meno (Crown) na utengenezaji wa taya zilizoathirika na ajali na magonjwa mbalimbali.

Utengenezaji wa meno, vifuniko vya meno na taya kwa kutumia teknolojia ya ‘3D Printing’ unatumia muda wa dakika 8 hadi 10, tofauti na sasa ambapo ili mtu atengenezewe jino au taya inachukua muda wa wiki mbili huku ikihusisha michakato mbalimbali ya kimaabara.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi alipokutana na uongozi wa Taasisi ya MCW kwa lengo la kujadili namna ya kuhakikisha huduma hiyo inaanzishwa haraka katika Hospitali ya Upanga na Mloganzila.

Prof. Janabi amemuagiza Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhavile na timu ya wataalamu mbalimbali kuhakikisha  mchakato wa ushirikiano huo unaharakishwa ili kufanya huduma hizi zianze kutolewa na wananchi wanufaike.

Alisema huduma hizi zikianza zitafanya Muhimbili (Upanga & Mloganzila) kuwa hospitali ya kwanza ya Umma nchini kutoa huduma hiyo ya kisasa .

“Kupitia ushirikiano huu wataalamu wetu watajengewa uwezo jambo ambalo litaendelea kuboresha huduma ya afya ya kinywa na meno na kurahisisha huduma ya utengenezaji wa meno bandia kwa watu wanaohitaji huduma hiyo,” alieleza Prof. Janabi

Kwa Upande wake mmoja wa viongozi wa Taasisi ya Miracle Corner, Bi Marion Bergman ameahidi kutoa ushirikiano kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa Muhimbili ili waweze kutoa huduma hiyo kwa ufanisi zaidi

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi