Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mtandao Ulaji Fedha Wabainika
Oct 25, 2023
Mtandao Ulaji Fedha Wabainika
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akipokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji
Na Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu, Mhe.  Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo imebainika watu 10 wanahusika na mtandao wa uhamishaji fedha kinyume cha taratibu.

“Taarifa nimeipokea na mapendekezo ya Kamati wote tumeyasikia. Hatua za haraka zichukuliwe kwa sababu Mhe. Rais anatafuta fedha za kuleta maendeleo lakini kuna watu wachache wanafanya ubadhirifu,” amesema.



Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo leo Oktoba 25, 2023 ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema kila mtumishi wa umma ni lazima atunze na kuratibu vizuri matumizi ya fedha zinazopatikana.

Amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wasiridhishwe na taarifa za miradi wanazopokea pindi wakiwa ziarani kwani licha ya kuwa kuna wataalamu wanatoa taarifa nzuri mbele ya viongozi hao, bado kuna michezo  wanachezacheza.

Akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Kigoma, Septemba 20-22, mwaka huu, Waziri Mkuu alipata taarifa ya uwepo wa fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ya Amana ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kutoka TAMISEMI na kisha fedha hizo kuondolewa baada ya muda bila maelekezo maalum wala kujua zilitumikaje.



“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti kwa muda halafu zinapotea, hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi TAMISEMI ili tuone huo mnyororo unaenda wapi,” alisema Waziri Mkuu wakati akizungumza na viongozi wa dini, Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma mjini Septemba 22, mwaka huu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi