Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mramba: Mwezi Agosti 2022 tunawasha umeme wa Gridi Kigoma
Jul 07, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Zuena Msuya, Kagera

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amewahakikishia wakazi wa Mkoa wa Kigoma kuwa Mwezi wa Agosti mwaka huu, mkoa huo utaanza kutumia umeme wa Gridi ya Taifa.

Mramba alisema hayo baada ya kukagua na kuona maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Nyakanazi na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Mradi wa umeme wa Rusumo wenye Msongo wa Kilovolti 400, alipofanya ziara Julai 6, 2022.

Mramba alisema katika bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023  ilieleza kuwa itapeleka umeme wa Gridi, katika mkoa huo.

Alisema kuwa Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wamefika katika hatua nzuri za ujenzi wa miradi hiyo na wanatarajia kukamilisha kazi hizo kabla ya mradi wa Rusumo kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.

“Nimekagua nimeona na nimejiridhisha kuwa wakandarasi hawa wanakwenda vizuri na nimewasisitiza wakamilishe miradi hiyo mapema iwezekanavyo ili wapate muda wa kufanya majaribio ya kutosha, na punde mradi wa Rusumo ukikamilika na kuanza kuzalisha umeme kusitokee changamoto ya aina yeyote”, alisema Mhandisi Mramba.

Alisema mradi wa Rusumo unahusisha nchi tatu ambazo ni Tanzania, Rwanda na Burund hivyo Tanzania inataka kuanza kutumia umeme huo mara tu baada ya kuanza kuzalishwa kwa kuwa uwezo wa kufanya hivyo inao, na haiko tayari kubaki nyuma.  

Aidha, alisema licha ya Nyakanazi kuwa chanzo cha kupeleka umeme Kigoma, baada ya kupokea umeme wa Rusumo pia kinapokea umeme wa Geita.

Alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa muda si mrefu, Mkoa wa Kigoma utakuwa na utajiri mkubwa wa umeme kuliko mikoa mingine kwa kuwa utapata umeme mwingi zaidi kutoka katika miradi mingi ya umeme inayoendelea kutekelezwa na kupita katika mkoa huo.

Alitaja miradi hiyo kua ni pamoja na huo wa Nyakazi ambao upelekaji umeme katika mkoa huo utafanyika kwa hatua mbili moja ya kupelekea umeme wa Kilovolti 33 ambao utaanzia katika kituo hicho hadi Kakonko na utakamilika mwezi huo wa Agosti , awamu ya pili ni upelekeaji wa umeme wa Kilovolti 400 ambao huo utakamilika mwezi Januari mwakani.

Umeme huo mkubwa utaungana na umeme unaotoka Sumbawanga, Katavi, hadi Kigoma, pia utaungana na umeme utakaotoka katika kituo kipya kinachojengwa Malagarasi kupitia Kidawe.

Aliweka wazi kuwa kwa Mkoa wa Kigoma kuingia katika Gridi ya Taifa hivi karibuni ni jambo ambalo litakuwa historia kwani watu hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo kwa miaka mingi iliyopita.

Hata hivyo alisema kuwa kuunga Mkoa wa Kigoma katika Gridi ya Taifa kutaipunguzia Serikali gharama kubwa iliyokuwa ikipata ya kununua mafuta mazito yaliokuwa yakitumika kuendesha kituo kidogo cha umeme katika mkoa huo.

Aliwataka wakazi wa Kigoma kujiweka tayari kuanza kutumia umeme huo katika shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa kuwa utakuwa ukipatikana kwa wakati wote na kupunguza adha ya kukatika mara kwa mara na wakati mwingine kupata umeme wenye nguvu ndogo.

Katika ziara hiyo Katibu Mkuu huo aliambatana na Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga na Maafisa wengine kutoka wizara hiyo na TANESCO.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Peter Kigadye alisema kuwa shirika hilo kwa sasa limeongeza jitihada za kuhakikisha kuwa umeme wa Gridi ya Taifa unafika katika mikoa yote ambayo bado haijafikiwa.

Na nguvu zaidi imeelekezwa katika kuhakikisha miradi ya kutatua changamoto za umeme inasimamiwa vyema na kutekelezeka ili kutimiza malengo yaliowekwa na TANESCO katika kuwahudumia Watanzania.

Kigadye alisema kupitia kituo cha Nyakanazi na njia ya kusafirisha umeme kutoka Rusumo hadi katika kituo hicho ni ushahidi tosha kuwathibitishia wananchi kuwa TANESCO na Serikali kwa ujumla imedhamiria kuondoa changamoto ya umeme kwa wananchi wake.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi