Na Zuena Msuya, Kagera
Mradi wa kuzalisha Umeme kwa kutumia nguvu ya maji ya Mto Kagera wa RUSUMO MW 80 utakamilika mwezi Novemba 2022 na kuanza kuzalisha Umeme utakaounganishwa na Gridi ya Taifa baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika kwa 95% hadi sasa.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba wakati wa ziara yao ya kikazi ya kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Mradi huo na hatua iliyofikiwa katika kutekeleza Mradi huo Mkoani Kagera, Julai 5, 2022.
Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Mramba amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo umefika 95% ya ujenzi wake na unatarajia kuanza uzalishaji wa Umeme ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Mradi huo unahusisha nchi tatu ambazo ni Tanzania, Rwanda pamoja na Burundi, unatarajiwa kuzalisha Megawati 80 za umeme ambazo utagawanywa katika viwango sawa katika nchi hizo.
Mhandisi Mramba alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza au kuondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya umeme katika mikoa yote ya kanda ziwa ikiwemo Kagera, Geita na Kigoma na maeneo mingine inayozunguka kanda hiyo.
Pia mradi huo ni muhimu kwa nchi hizo tatu kwa kuwa utaongeza uzalishaji wa umeme katika Ukanda wa Afrika Mashariki na hivyo kuimarisha huduma ya upatikanaji wa umeme katika ukanda huo.
“Ujenzi wa maeneo yote muhimu ya Mradi huo ambayo ni Tuta Kuu, nyumba ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme, Kituo cha kupoza na kuchochea umeme, Handaki la kupeleka maji katika mitambo ya kuzalisha umeme, ufungaji wa mitambo pamoja na nyumba 24 za watumishi watakaofanya kazi katika kituo hicho zimekamilika na kinachofanyika sasa ni kukamilisha kazi ndogondogo”, alisema Mhandisi Mramba.
Mradi huo pia umetekeleza shughuli za kijamii kwa kujenga vituo vya afya, Zahanati, Maabara, vyumba vya madarasa na mabweni ya shule za msingi na sekondari, mabwalo ya chakula, miundombinu ya maji, kuwawezesha kilimo vitalu, na kuwezesha ufugaji wa mbuzi, nyuki, Ng’ombe, na Sungura katika wilaya zinazozunguka mradi huo.
Wilaya hizo ni Ngara kwa upande wa Tanzania, Kirehe na Ngoma kwa upange wa Rwanda na Busoni kwa upande wa Burundi, miradi iliyogharimu takribani Dola za kimarekani milioni 5 kwa kila nchi.
Pamoja na Mambo mengine Mhandisi Mramba amewataka wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu pembeni mwa vyanzo vya maji katika mito inayomwaga maji Mto Kagera kuacha mara moja shughuli hizo na kuondoka maeneo hayo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya mradi huo pamoja na kuitunza kwa manufaa yao wenyewe na taifa kwa jumla.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, amesema kuwa mradi huo unatekelezwa katika sehemu kuu mbili, ambazo ni ujenzi wa miundombinu ya mitambo wa kuzalisha umeme na njia ya kusafirisha umeme ambapo fedha za kutekelezwa mradi huo zimetolewa Benki ya Dunia (WD) pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika( AfDB).
Tutuba aliweka wazi kwamba hadi sasa malipo ya fedha za kutekeleza mradi huo yanaendelea kufanyika vizuri na amewatoa hofu watanzania kuwa mradi huyo utaanza uzalishaji wa umeme ifikapo mwezi Novemba mwaka huu kwa kuwa fedha za kukamilisha malipo ya kazi iliyobaki zipo tayari.
“Mradi huo ni kielelezo kikubwa cha ushirikiano baina ya nchi Tatu ambazo ni Tanzania, Rwanda na Burundi zitakazokuwa zikitumia Umeme unaozalishwa katika Mradi huo kwa kugawana kiwango sawa cha Megawati 26.6 za Umeme kwa kila nchi, hivyo ni jukumu la kila serikali husika kuhakikisha fedha zilizotolewa kufadhili utekelezaji wa mradi wa Rusumo zinatumika ipasavyo”, alisisitiza Tutuba.
Ujenzi wa kusafirisha umeme wa Kilovolti 220 katika mradi huo ili ziunganishwe katika Gridi ya Taifa kwa nchi hizo tatu, itaanzia Rusumo hadi Gitega kwa upande wa Burundi urefu wa Kilometa 109, Rusumo hadi Kigali kwa upande wa Rwanda Kilomita 160, Rusumo hadi Nyakanazi Kilomita 94 kwa upande wa Tanzania.
Wafanyakazi wa RUSUMO wamegawanyika katika makundi mawili, moja la vibarua na wafanyakazi wa muda mfupi, na pili wafanyakazi wa kudumu, katika mradi huo, mpaka sasa wafanyakazi wakudumu kwa kada za taaluma mbalimbali ni 36, ambapo kila nchi imetoa wafanyakazi 12.