Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mradi wa “HEET” Waendelea kwa Kasi Mzumbe
Oct 21, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu Mratibu wa Mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu Kiuchumi ‘HEET’, Dkt. Hawa Tundui, amepongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na wadau mbalimbali wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kutekeleza kwa kasi malengo yaliyowekwa katika Mradi wa HEET.

Hayo ameyasema wakati akifungua kikao kazi cha siku nne cha  wataalamu wa TEHAMA, wahadhiri na wadau muhimu katika sekta ya utoaji mafunzo kwa njia ya mtandao “Elimu Masafa”, wanaokutana kutathmini mahitaji na mapungufu ya mfumo huo kwa sasa kwa kuzingatia mahitaji na malengo ya mradi ambao umejikita katika kuboresha matumizi ya TEHAMA.

Dkt. Hawa amewahimiza washiriki wa kikao hicho kutumia taaluma zao kuhakikisha vipengele vyote muhimu vya kuweka mifumo thabiti ya TEHAMA kulingana na vipaumbele vya mradi vinazingatiwa ili kufikia malengo mapana ya mradi ambayo ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kujiunga na elimu ya juu na kuinua kiwango cha matumizi sahihi ya TEHAMA katika kufundisha.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Dkt. Isaya Lupogo, Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi za Huduma za Jamii amesema, mradi wa “HEET” umekuja wakati muafaka ambapo elimu masafa inahitajika sana kutokana na kuongezeka kwa kasi kubwa ya matumizi ya teknolojia katika ufundishaji duniani unaotegemea zaidi teknolojia.

Naye Mratibu wa kikao hicho, Dkt. Perpetua Kalimasi, amesema kikao hicho cha siku nne, kimelenga mbali na kufanya tathmini ya mifumo ya utoaji elimu masafa iliyopo, kuangalia njia bora za kuboresha na kuanzisha mifumo mipya ya utoaji mafunzo ya Elimu Masafa, na kuandaa kikao kikubwa kwa wadau wanufaika wa moja kwa moja wa Elimu masafa, ili kukusanya maoni na kuunda mifumo ya thatmini ili mradi wa “HEET” uwe na matokeo yaliyokusudiwa kwa wadau. 

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha TEHAMA cha Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Mohamed Ghasia, amesema mbali na kuboresha na kuanzisha mifumo ya utoaji elimu kwa njia ya masafa, mradi wa “HEET” kupitia Kitengo cha TEHAMA, kimejizatiti kuimarisha na kuongeza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA, kupanua wigo wa matumizi ya mifumo kidigitali, kutoa elimu kwa wadau wote pamoja na kuboresha miundombinu ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya dunia.

Kikao kazi hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mradi ‘HEET’, ulioanza kutekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi