Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mongella: Royal Tour Yazidi Kumimina Watalii Arusha
Sep 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Immaculate Makilika – ARUSHA

Filamu ya “The Royal Tour” inayotangaza vivutio vya utalii imeendelea kuleta manufaa mbalimbali nchini hususan jijini Arusha kwa kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini.

Akizungumza leo jijini hapa na ujumbe wa Idara ya Habari – MAELEZO, ulioongozwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella ameeleza kuwa kumekuwepo na faida lukuki za filamu hiyo.

“Utalii unaendelea vizuri na watalii wengi wameendelea kuja Arusha, mfano magari yanayofika Ngorongoro Crater sasa yanafika 700 kwa siku moja, na hali hii inaweza kuleta changamoto kwa mazingira ya wanyama na hivyo tumeanza kufikiria tofauti ili kulinda mazingira katika maeneo yetu ya utalii". Ameeleza Mhe. Mkuu wa Mkoa.

“Katika Uwanja wa Ndege wa Arusha watalii wamekuwa wengi ambapo kwa siku moja si chini ya miruko 100 ya ndege na wasafiri zaidi ya asilimia 80 ni watalii. Mwaka huu ndege za kimataifa ni nyingi mno, na wataalamu wa masuala ya utalii wanasema kipindi kijacho watalii wataongezeka zaidi kwa vile hawa wanaokuja wengi wao ni wale waliolipia tangu mwaka 2020 kuja kutalii nchi,” amesema Mhe. Mongella.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa ameeleza kuwa Filamu ya “The Royal Tour” ni mkakati wa Serikali katika kutangaza vivutio vyake vya utalii duniani ili nchi iweze kuongeza mapato yake yanayopatikana kupitia sekta hiyo ya utalii nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi