Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

MKURABITA Yashusha Neema Kwa Wananchi Butiama
Oct 22, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Maalum – BUTIAMA

Mpango wa Kurasimisha Rasilimali  na Biashara  Tanzania( MKURABITA) umekabidbi zaidi ya hati miliki za kimila 515 kwa wakazi wa vijiji vya Nyakiswa na Kyankoma wilayani Butiama mkoani  Mara baada ya MKURABITA kuendesha zoezi la upimaji ardhi katika vijiji hivyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Akizungumza kwenye hafla ya kutoa hati hizo hivi karibuni, mwakilishi wa mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Alphonce  Mlelwa amesema kuwa, hati hizo zinawasaidia wananchi kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kwamba kati ya hati zilizotolewa, 341 ni za Wakazi wa Kijiji cha Nyakiswa na 174 za Kijiji cha Kyankoma.

“Tumeendelea kushuhudia Serikali ya Awamu ya Tano ikifanya kazi kubwa kuwezesha makundi mbalimbali pamoja na kuwapimia mashamba haya na kuwapatia hati ili wananchi waweze kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi”, alisema

Mlelwa ameeleza kuwa, utekelezaji wa Mpango huo utawawezesha wananchi kujiletea maendeleo endelevu na kuchangia katika kukuza uchumi.

Kwa upande wake, Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia  Mgembe amesema kuwa kati ya hati hizo 135  ni za wanawake huku baadhi ya hati zikimilikiwa kwa panoja kati ya  mke na mume, hatua inayolenga kuwakwamua wananchi wote kiuchumi kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

“Serikali imeamua kutoa hati hizi ili kuboresha maisha ya wananchi wake wote hasa wa vijijini kwa  kuwa hati hizi ni mojawapo ya kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi  hivyo nawaomba wananchi wote kuzitumia katika kujiendeleza kiuchumi sambamba na kuendeleza maeneo yaliyopimwa ili kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na maeneo yao kwa ujumla,” Alisisitiza

Dkt. Mgembe amesema mbali na faida za kiuchumi, kutolewa kwa hati hizo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia na hata  kumaliza kabisa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikitokea katika baadhi ya maeneo nchini.

Nae, Meneja Urasimishaji Rasilimali Ardhi Vijijini, Bw. Antony Temu amesema, " Tunaamini kuwa tukiendesha zoezi hili katika vijiji vya mfano,vijiji vilivyobaki vitaona faida na kisha kuishikiniza  halmashauri yao kufanya upimaji hatua ambayo ina manufaa makubwa".

Pamoja hayo, amesema Mpango huo umekuwa ukiwajengea uwezo wananchi kuhusu namna bora kutumia hati hizo na baada ya mafunzo hayo wanaamini kuwa wakazi hao wataongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi kwani zitawawezesha kupata mitaji kwa kutumia hati hizo ambapo changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa wananchi vijijini itakwisha kabisa.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa hati hizo, baadhi ya wanufaika wa mradi huo waliushukuru mpango huo na kusema kuwa hati hizo zitasaidia katika kupata maendeleo endelevu.

Bw. Nelson Msamba amesema wakazi wengi wa vijiji hivyo walikata tamaa baada ya kushindwa kupewa hati hizo kwa wakati baada ya kukamilika kwa upimaji, lakini hivi sasa matumaini yao yamefufuka baada ya kuzipokea na kwamba wanatarajia kuanza kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa uhakika zaidi kwavile uhakika wa kupata mitaji hivi sasa wanao.

MKURABITA tayari imezifikia zaidi ya Halmashauri 50 nchini hapa na kufanya urasimishaji ardhi na biashara ikiwa ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali  katika kuwawezesha wananchi..

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi