Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema Mkongo wa Baharini wa 2Afrika utaongeza kasi ya intaneti nchini zaidi ya mara kumi ya intaneti iliyopo sasa.
Mhe. Nape amesema hayo leo Agosti 10, 2023 wakati wa uzinduzi wa mkongo mkubwa wa mawasiliano wa baharini wa 2Afrika na huduma ya intaneti ya kasi ya 5G ya Airtel Tanzania.
“Mkongo huu utaongeza kasi ya intaneti nchini kwetu zaidi ya mara kumi ya sasa, ubora wa intaneti nchini utaongezeka sana, utasaidia katika jitihada za kushusha gharama za mawasiliano nchini, ni fursa kubwa ya kuvutia uwekezaji wa makampuni makubwa duniani kama vile Google, Meta na Netflix,” amesema Mhe. Nape.
Ameendelea kusema kuwa, mkongo huo utakuza uchumi wa nchi pamoja na kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania.
Aidha amesema kuwa, mkongo huo umejengwa kwa teknolojia ya kisasa, hivyo una sifa ya kuwa na kasi kubwa zaidi.
Mkongo wa Baharini wa 2Afrika ndio mkongo mrefu na mkubwa kuliko mikongo yote duniani. Mkongo huu una urefu wa KM 45,000, unaunganisha zaidi ya nchi 33 duniani, unaunganisha mabara matatu, Afrika, Asia na Ulaya. Mkongo huo unategemea kuunganisha zaidi ya watu bilioni 3 duniani.