Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mkakati Shirikishi wa Kulinda Urithi wa Ukombozi wa Afrika Wasukwa
Jan 29, 2024
Mkakati Shirikishi wa Kulinda Urithi wa Ukombozi wa Afrika Wasukwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa leo Januari 29, 2024 ameongoza kikao cha pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara tano cha kujadili mkakati shirikishi wa Kulinda, Kuhifadhi na Kuendeleza Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika uliopo nchini.
Na Shamimu Nyaki

Makatibu Wakuu wa Wizara tano leo Januari 29, 2024 wamefanya  kikao cha pamoja  kujadili mkakati shirikishi  wa Kulinda, Kuhifadhi na Kuendeleza Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika uliopo nchini.

Mkakati huo unajadiliwa kwa kuzingatia kuwa Tanzania ndio iliyopewa dhamana ya kuulinda na kuhifadhi Urithi huo na Nchi Wanachama Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2011 kupitia azimio la kuanzisha Programu mahsusi ya kuhifadhi kumbukumbu za Ukombozi wa Afrika.

Kikao hicho ambacho kimeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa ambapo pamoja na mambo mengine, kimepitia mambo muhimu kuhusu mkakati huo kuhakikisha Tanzania kama mwenyeji wa Urithi wa Ukombozi inakuwa ni ajenda ambayo inashirikisha wadau mbalimbali pia kuhakikisha maeneo ya Urithi wa ukombozi ambayo yanapatikana nchini yaweze kuinufaisha Tanzania na nchi wanachama wa Programu hiyo.

Aidha, lengo la mkakati huo ni kuhakikisha wizara na taasisi ambazo zinahusika kwenye mkakati huo ambazo ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Elimu, Maliasili na Utalii, Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ofisi ya Rais -TAMISEMI zinatekeleza Programu hiyo.

Vilevile, kuwa na jukumu la kushiriki, kulinda na kuhifadhi kumbukumbu za Ukombozi ili Kituo hicho kiongeze wigo wa uhifadhi wa Urithi wa Ukombozi wa Afrika.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Farasi Mnyepe, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Said Mussa, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Franklin Rwezimula, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Sospeter Mtwale na mwakilishi kutoka  Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Antony Mwijage na Wataalamu mbalimbali kutoka wizara hizo, kinatanguliwa na kikao cha ngazi ya Mawaziri ambacho kitajadili mapendekezo ya maazimio ya kikao hicho na kutolea maamuzi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi