Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Miradi ya REA ni ya Wananchi - Wakili Kilolo
Jun 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Veronica Simba  - REA

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo amesema wananchi wana haki ya kujulishwa kuhusu miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika maeneo yao kwani kimsingi miradi hiyo ni ya kwao.

Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti hivi karibuni akiwa katika ziara ya kazi mkoani Tanga, Juni 13 hadi 16, 2022 ambapo alifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.

Akifafanua, Mwenyekiti wa Bodi alisema Serikali imewekeza fedha nyingi katika kutekeleza miradi hiyo ambayo imelenga kuwanufaisha wananchi hususan waishio vijijini.

“Kwa mantiki hiyo, wananchi ndiyo wamiliki wa miradi husika; miradi ni ya kwao maana inatekelezwa na Serikali kwa ajili yao hivyo wanapaswa kuijua vizuri ili watoe ushirikiano katika utekelezwaji wake,” alisisitiza.

Aidha, Wakili Kalolo alisema kuwa endapo Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo watawashirikisha wananchi, itasaidia pia kupata suluhisho la changamoto ya uharibifu na wizi wa miundombinu ya umeme ambayo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo.

Alisema kuwa, wananchi wakishirikishwa watakuwa sehemu ya Mradi hivyo watatoa ushirikiano katika usimamizi wake ikiwemo utunzaji wa miundombinu.

Aliongeza kuwa ushirikishwaji uwalenge pia viongozi wa wananchi ambao ni Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wabunge, Madiwani na viongozi wote ngazi ya vijiji na vitongoji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Saidy akizungumza katika ziara hiyo aliwataka wananchi kuondoa hofu kuhusu suala la wigo wa miradi ya umeme vijijini, ambapo kumekuwa na malalamiko ya umeme kufika eneo dogo katika kijiji na maeneo mengine kutofikiwa.

Alifafanua kuwa, malengo ya Serikali katika hatua ya awali ilikuwa ni kuhakikisha walau kila kijiji kinafikiwa na miundombinu ya umeme mkubwa ili upatikanaji wa huduma za msingi hususan za kijamii ziwepo katika kila kijiji.

Mhandisi Saidy aliongeza kuwa, kwa sasa Serikali imejipanga kuongeza wigo ambapo katika kila kijiji zitaongezwa kilomita mbili kutoka kilomita moja ya awali, hivyo kufikia kilomita tatu.

Aidha, alisema kuwa Wakala unaendelea kutekeleza miradi mingine mbalimbali inayolenga kuendelea kuwafikishia umeme wananchi wote ikiwemo miradi ya ujazilizi.

Pia, alibainisha kuwa mpango wa Serikali kwa sasa kupitia REA ni kuanza kupeleka umeme katika ngazi ya vitongoji ambapo ukikamilika, wananchi wote watakuwa wamefikiwa na nishati ya umeme.

Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali walipongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali kupitia REA na wakaahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuwezesha utekelezaji wa miradi inayoendelea.

Viongozi hao ni pamoja na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Adam Malima, Mbunge wa Handeni Vijijini Mhe. John Sallu, Msaidizi wa Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwemkola, Mhe. Hozza Mandia, na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni ambaye ni Katibu Tawala, Mashaka Mgeta.

Wengine ni Diwani wa Kata ya Mponde, Mhe. Richard Mbuguni, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga ambaye ni Katibu Tawala, Joseph Sura, Afisa Mtendaji Kata ya Mwakijembe, Prosper Marumbo, Mwenyekiti wa kijiji cha Msomera wilayani Handeni Martin Parakett na viongozi wengine mbalimbali ngazi ya vijiji na vitongoji.

Ziara hiyo ya siku tatu ililenga kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini ikihusisha kukagua kazi zinazoendelea pamoja na kuzungumza na wakandarasi, viongozi na wananchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi