Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Milioni 187.5 Zatumika Kununua Vifaa vya Ukalimani Kukuza Kiswahili
Aug 23, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na. Georgina Misama - MAELEZO.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali imetumia kiasi cha shilingi milioni 187.5 kununua vifaa vya kisasa vya kufundishia ukalimani vifaa ambavyo vitaliwezesha Baraza la Taifa la Kiswahili (BAKITA) kutoa mafunzo ya msasa na kuwasajili wakalimani watakaotumiwa katika mikutano mbalimbali kitaifa na kimataifa.

Mhe. Bashungwa amesema kununuliwa kwa vifaa hivyo kumetimiza miongoni mwa malengo ambayo Serikali ilijiwekea katika kukuza lugha ya Kiswahili kwani kinawaunganisha Watanzania kuwa wamoja katika shughuli mbalimbali ambazo wanashiriki kama Taifa.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa vifaa hvyo iliofanyika leo jijini Dar es salaam katika Ofisi za BAKITA, Mhe. Bashungwa amesema Kiswahili hivi sasa kinazidi kuenea kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwani kinatumia katika vyombo mbalimbali vya habari duniani, kufundishwa katika shule, vyuo na taasisi nyingine za elimu za kimataifa na hata kwa mtu mmoja mmoja katika mataifa mengi duniani.

“Chimbuko la Kiswahili ni hapa kwetu Tanzania, tuna wajibu mkubwa wa kukiendeleza zaidi kwa kuwasaidia wengine wanaokitafuta kwa kuwapatia rasilimali mbalimbali zitakazo wawezesha kukielewa na kukitumia kwa usanifu na ufasaha zaidi. Moja ya rasilimali hizo muhimu ni utaalamu huu wa ukalimani,” alisema Bashungwa.

Aidha, Mhe. Bashungwa ameitaka BAKITA kutumia vifaa hivi kwa ajili ya kuwaandaa wakalimani wa kutosha ili nchi iwe na uwezo wa kuwapeleka katika mikutano mbalimbali kulingana na mahitaji ya kimataifa kwani hii ni fursa ya Watanzania kujiuza kimataifa hasa wakati huu ambao Serikali ipo katika mchakato wa kubidhaisha lugha hiyo.

Wakati huo huo ametoa rai kwa Watanzania wenye utaalam wa ukalimani na wanaojua lugha za kimataifa kama vile Kiingereza, Kireno, Kichina, Kifaransa, Kijerumani na Kiarabu kutumia fursa hiyo kwa kwenda BAKITA kupata mafunzo ya msasa ya kutumia vifaa vya ukalimani na kijisajili ili Serikali iweze kutambua idadi ya wataalam ilionao na pia kuweza kuwapeleka katika mikutano ya kimataifa pindi mahitaji hayo yatakapowasilishwa.

Mhe. Bashungwa pia amewataka wataalamu wengine wa Kiswahili wakiwemo wafasihi, walimu wa Kiswahili kwa wageni na wahariri ambao bado hawajajisajili katika kanzidata ya BAKITA, kufanya hivyo haraka iwezekanavyo ili kuwekewa utaratibu mzuri wa kuwawezesha kupata fursa za Kiswahili zinazojitokeza nje ya nchi na kuwaahidi Watanzania wote wenye weledi wa Kiswahili kufaidika nacho.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesema ni wakati sasa wa BAKITA kufanya tafsiri ya kanuni na miongozo mbalimbali ya kisheria kuwa katika lugha ya Kiswahili kitu ambacho kitawawezesha Watanzania wengi kushiriki katika mambo yanayowahusu bila ya changamoto ya uelewa wa lugha.

“Nilipata nafasi ya kupita hapa katika ziara zangu kwa taasisi za wizara, napenda tu kuwakumbusha myafanyie kazi yale tuliyokubaliana likiwepo suala la kufanya tafsiri ya kanuni na miongozo ya kisheria kuwa katika lugha ya Kiswahili, tuanze na kanuni muhimu katika wizara yetu. Sheria na miongozo mingi inawahusu watanzania wa kawaida ni vizuri ikawekwa kwa Kiswahili ili wahusika waielewe”, alisema Mhe. Gekul.

Akitoa neno fupi Kaimu Mtendaji wa baraza hilo, Bi Consolata Mushi alisema kwamba vifaa  hivyo vitatumika  kwa manufaa ya kundi kubwa la Watanzania kwani vitatumika pia na vyuo vyenye uhitaji kwaajili ya kufundishia mazoezi ya vitendo.

“Ninawaahidi kwamba vifaa hivi vitatunzwa na kutumika kwa namna iliyokusudiwa na Serikali yetu, hakutakuwa na matumizi mengine yoyote yasiyokuwa na tija kwa  Serikali na Umma wa tawanzania, aidha, Baraza linaruhusu vyuo vikuu vya hapa nchini kutumia vifaa hivi kwaajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa ukalimani kwani baadhi ya vyuo vyetu havina vifaa hivi hivyo wanafunzi hufundishwa nadharia pekeyake,” alisema Bi. Consolata.

Vifaa hivyo vilivyozinduliwa leo vinajumuisha chombo maalum kwaajili ya kuchagua lugha na kuzungumza,seva, vipaza sauti, visikika na spika. Vifaa vingine ni pamoja na kikuza sauti na mashine ya mkalimani ambavyo vitawezesha jumla ya lugha nane kufanyiwa ukalimani kwa wakati mmoja lakini pia vinaweza kutumiwa na watu 30 kwa wakati mmoja.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi