Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mikataba ya Bilioni 60.3 ya Ujenzi na Ukarabati wa Vivuko Yasainiwa
Oct 18, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Alfred S. Mgweno (TEMESA)

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imesaini mikataba yenye thamani ya Shilingi bilioni 60.3 kwa ajili ya ujenzi wa vivuko vipya, ukarabati wa vivuko vinavyoendelea kutoa huduma ambavyo muda wake wa ukarabati umefikia pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vivuko kote nchini.

Hayo yamebainishwa leo wakati wa hafla fupi ya uwekaji wa msingi (Keel Laying) wa ujenzi wa kivuko kipya kitakachokuwa kinatoa huduma kati ya Kisorya wilayani Bunda mkoani Mara na Rugezi wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, hafla iliyofanyika katika yadi ya Songoro iliyopo Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amepongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa kuanza Ujenzi wa Kivuko hicho na kuwataka kuhakikisha kinakamilika kwa haraka na kwenda kutoa Huduma katika maeneo ya Kisorya na Rugezi.

“Nafurahi kusikia kuwakazi ya ujenzi wa kivuko kipya cha Kisorya - Rugezi uko katika hatua za kuanza kujengwa kwa gharama za kitanzania jumla ya Shilingi Bilion 5 ikiwa imetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Sina budi kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza Ujenzi huu.” Alisema Mkuu wa Mkoa na kuongeza kuwa ujenzi wa kivuko kipya cha Kisorya – Rugezi utachochea na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi wa maeneo zitakapoenda kutoa huduma.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Lazaro Kilahala, akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa kivuko hicho amesema, katika mwaka huu wa fedha Wakala unaendelea na ujenzi wa vivuko vipya vitano ambavyo ni Kisorya - Rugezi, Bwiro – Bukondo, Nyakalilo – Kome, Ijinga – Kahangala na Mafia Nyamisati.

“Mikataba yenye thamani ya Shilingi bilioni 33.2 imeshasainiwa, Wakandarasi wameshalipwa malipo ya awali na kazi inaendelea, miradi mingine ni vivuko vya Buyagu-Mbalika na Magogoni-Kigamboni ambavyo viko katika hatua za manunuzi.” Alisema Mtendaji Mkuu

Ameongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha, Serikali inavifanyia ukarabati vivuko 14 vya MV. KAZI, MV. MISUNGWI, MV. MUSOMA, MV. SABASABA, MV. TANGA, MV. NYERERE, MV. KITUNDA, MV. KILOMBERO II, MV. RUHUHU, MV. OLD RUVUVU, MV. MAGOGONI, MV UJENZI, MV KOME II na MV MARA kwa gharama ya Shilingi bilioni 22.99 na ukarabati wa miundombinu ya vivuko katika maeneo 11 kwa gharama ya Shilingi bilioni 4.1.

Mtendaji Mkuu ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha kifedha kutekeleza mradi huo na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na jitihada kubwa ili kufikia malengo na matarajio ya Serikali na wananchi kwa ujumla. Kivuko hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 sawa na tani 170.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi