Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Miaka Miwili ya Serikali ya JPM Yaleta Mageuzi Makubwa
Nov 05, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_21783" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Usajili, Patrick Kipangula na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Habari na Picha, Rodney Thadeus.[/caption]

Na Ismail Ngayonga.

SERIKALI imesema Tanzania imefanikiwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na kuimarika kwa mifumo ya uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari akielezea kuhusu Mafanikio ya miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa Mataifa mbalimbali duniani yamekuwa yakiimwagia sifa Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na udhubutu na hatua yake ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani, jambo ambalo limeshindwa kutekelezwa na mataifa mbalimbali ya Bara la Afrika.

[caption id="attachment_21784" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi (katikati) wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli mapema hii leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Idara ya Habari - MAELEZO).[/caption]

Akitolea mfano Dkt. Abbasi anasema, hadi kufikia sasa Serikali tayari imetenga kiasi cha shilingi Trilioni 1.9 za mapato yake ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) hatua inayolenga kurahisisha shughuli za usafiri pamoja na kuchagiza shughuli za uchumi na maendeleo ya wananchi.

Dkt. Abbasi alisema katika kipindi cha miwili ya utawala wa Rais Magufuli, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kutekeleza ahadi mbalimbali ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi pamoja na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji umeme na barabara.

“Tangu kuingia Madarakani, Serikali imeongeza bajeti yake katika sekta muhimu, mfano katika afya Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza bajeti ya dawa na vifaatiba kazi kutoka Shilingi Bilioni 30 mwaka 2015 hadi Tsh. Bilioni 261 mwaka 2017 pamoja na kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka Tsh Bilioni 48.6 mwaka 2015 hadi Bilioni 461 mwaka 2017” alisema Dkt. Abbasi.

Anasema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inajitegemea kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa makusanyo wa fedha za ndani, ambapo katika kipindi cha miaka miwili makusanyo yameweza kuongezeka kutoka Tsh. Trilioni 9.9 mwaka 2015 hadi Trilioni 14 mwaka 2017.

Aidha Dkt. Abbasi anasema Serikali ya Awamu ya Tano kuwa imepata mafanikio makubwa kutokana kupunguza bajeti ya matumizi ya safari kwa Viongozi na Maafisa kusafiri nje ya nchi kutoka Tsh, Bilioni 216 mwaka 2014/15 hadi kufikia Tsh. Bilioni 25 kati ya mwaka 2015-17, ambapo fedha hizo zimeweza kutumika katika kutwekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dkt. Abbasi anasema katika kutetea na kutekeleza ajenda ya maendeleo kwa wananchi wake, Serikali ya Awamu ya Tano tayari imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya madini, ambapo katika mazungumzo yaliyofikiwa hivi karibuni baina ya Serikali na Kampuni ya Barrick, Serikali itaweza kupata hisa ya asilimia 16 na mgawanyo wa asilimia 50/50 wa faida.

Akifafanua zaidi Dkt. Abbasi anasema kutokana na juhudi na mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano, Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) limeitaja Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Mataifa ya Afrika Mashariki kuvutia Wawekezaji kwa kuwa na mtaji wa Dola Bilioni 1.35 .

Dkt. Abbasi aliwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi na jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuboresha na kuinua na kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi wa hali ya chini.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi