Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe ameutaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kutobweteka na maboresho ya kimfumo na badala yake kuweka mkakati wa kuhakikisha wanakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Mhe. Kigahe ametoa agizo hilo leo Oktoba 25, 2024 wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni na wadau wake uliofanyika kwa siku moja jijini Dar es Salaam.
Mhe Kigahe amesema anatambua kuwa kuanzia mwaka 2018 BRELA imekuwa ikitoa huduma zake za Sajili na Leseni kwa njia ya mtandao ambayo imepunguza muda, gharama na bughudha kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
"Utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao umerahisisha mambo mengi, wafanyabiashara wanaweza kuomba kusajili au kupata Leseni za Biashara zao wakiwa maofisini kwao na wakapata cheti cha Usajili au Leseni pale walipo bila kuhitaji kufika katika ofisi za BRELA, jitahidini kuendelea kwenda sambamba na teknolojia kwani hii inafanya huduma yenu izidi kuwa bora na wezeshi," amesema Mhe. Kigahe.
Ameongeza kuwa, BRELA wanafanya maboresho ya mifumo yake ya Usajili na Utoaji wa Leseni ili kuondoa changamoto zilizobainika katika mifumo iliyopo sasa na kuja na mfumo mpya ambao utaongeza kasi, ufanisi na usalama wa taarifa za sajili, leseni na wawekezaji nchini, hivyo ni matarajio ya Serikali kwamba maboresho hayo yatapunguza zaidi muda na masaa ya sajili na leseni kuwa ndani ya masaa machache, kuongeza kasi ya urasimishaji wa biashara na kuongeza idadi ya wawekezaji na wafanyabiashara na hivyo kuongeza wigo wa ajira na walipa kodi.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya BRELA, Prof. Neema Mori amesema kuwa Kauli mbiu ya mkutano huu "Mifumo ya Kitaasisi Inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara Nchini" inaendana na ufanyaji kazi wa BRELA kwani huduma zinazotolewa na BRELA zinaweza kusomana na taasisi mbalimbali nchini.
"Bodi ya Ushauri ya BRELA itaendelea kusimamia na kutoa ushauri wa jinsi ya kuongeza ufanisi, hadi sasa bodi imeweza kufanikisha kuongeza mapato ya BRELA na hatimaye kutoa gawio la shilingi bilioni 18 kwa serikali." Amemalizia Prof. Neema.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa amesema BRELA imeandaa maonesho na mkutano wa wadau kwa lengo la kujadili mafaniko, fursa na changamoto zinazohusu sajili mbalimbali zinazotolewa pamoja na urasimishaji wa biashara kiujumla.
"Uwepo wa Taasisi za Umma na Binafsi kwenye mkutano huu wa pili wa BRELA na wadau wake utasaidia kujadili mafanikio, fursa na changamoto za Sekta ya Biashara." Amesema Nyaisa.