Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mhe. Kapteni Mstaafu George Mkuchika Azindua Mwongozo wa Utekelezaji wa Shughuli za Ustawi wa Jamii
Sep 23, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na WMJJWM, Dodoma


Akizindua mwongozo huo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Mhe. Kapteni Mstaafu George Mkuchika amesema, Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amezitaka Wizara zinazohusika na utekelezaji wa Mwongozo wa Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii kuhakikisha zinasimamia urasimishwaji na utekelezaji wa mwongozo huo katika jamii.


Hayo yamebainika wakati wa uzinduzi wa Mwongozo huo uliofanyika leo Septemba 23, 2022 jijini Dodoma ambapo Mhe. Mkuchika ameeleza kuwa utekelezaji wa Afua za Ustawi wa Jamii ni suala mtambuka linalotekelezwa na Wadau tofauti hivyo mwongozo huo utatumiwa na Wadau wa kisekta wanaotoa Huduma za Ustawi katika kuhakikisha Mipango na bajeti zao zinaakisi Mipango na vipaumbele vya Serikali.


"Mwongozo huu pia utasaidia katika upangaji wa Mipango, bajeti pamoja na upatikanaji wa taarifa mbalimbali zinazowahusu watoto, watu wenye ulemavu, wazee na Makundi Maalum" amesema  Mhe. Mkuchika.


 Ameongeza kuwa utekelezaji wa mwongozo huu utachochea kwa kiasi kikubwa kasi ya utoaji na upatikanaji wa Huduma Bora za Ustawi wa Jamii kwa Makundi Maalum na hivyo kujenga mustakabali imara wa Jamii ya kitanzania katika kufikia matarajio yao.


Aidha, Mhe. Mkuchika amesema mwongozo huo utaimarisha mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za Huduma za Ustawi wa Jamii na kujumuishwa katika mfumo wa kidijitali wa mipango na taarifa.


Ameziagiza pia Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kukusanya takwimu na kuandaa mipango na bajeti za Ustawi wa Jamii kwa mujibu wa mwongozo huo.


"Mwongozo usimamiwe kikamilifu ili kuwezesha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikumba Jamii ikiwemo ukatili wa kijinsia hasa wanawake na watoto, mauaji na matukio ya kujiua katika Jamii na ongezeko la watoto wa mitaani", alisisitiza Mhe. Mkuchika 


Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema lengo la kuzindua mwongozo huo ni kuimarisha utoaji wa huduma kwa Makundi Maalum ikiwemo wazee, walemavu, watu wenye magonjwa sugu, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na makundi mengine yenye mahitaji maalum.


"Kumekuwa na ukatili mwingi unaoendelea kwenye jamii na kazi kubwa inafanywa kuhakikisha wananchi wanaelewa haki zao tofauti na mwanzo, tumeenda mbele zaidi tuna jeshi la jamii linayojulikana kama SMAUJATA, nitoe wito kwa wananchi kujiunga na niwapongeze Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii kwa kazi kubwa" amesema Mhe. Dkt. Gwajima.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Sinyamule ameshukuru kwa niaba ya watekelezaji wa mwongozo huu na kusema kwamba utakuwa kitendea kazi muhimu kwa wao kufanyia kazi ili kuhakikisha Makundi Maalum yanapata huduma zinazostahili. 

"Nazipongeza Wizara kwa kuanzisha mwongozo huu ambao utaunganisha sekta mbalimbali katika kutatua changamoto za Makundi haya", amesema Mhe. Sinyamule.


Mwongozo huu unatekelezwa na Wizara Taasisi na wadau mbalimbali wa maendeleo zikiwemo Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Fedha na Mipango, Mambo ya Ndani ya Nchi, Katiba na Sheria, Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Afya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi