Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mfumo wa Epicor 10.2 Kuimarisha Ukusanyaji wa Mapato
Jun 05, 2018
Na Msemaji Mkuu

 Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Bw. Diwani Athumani akifungua mafunzo kwa maafisa usimamizi wa fedha kwa Mikoa ya Kigoma na Kagera yanayofanyika Bukoba Mkoani Kagera.

Na: Nashon Kennedy- Kagera

WATALAAM na wasimamizi wa fedha wa halmashauri nchini wametakiwa kuwa na usimamizi mzuri wa mifumo ya fedha  ili iweze kuleta ufanisi na utendaji kazi ikiwemo ukusanyaji wa uhakika wa mapato ya halmashauri.

Agizo hilo limetolewa jana mjini hapa  na Katibu Tawala wa Mkoa  wa Kagera Diwani Athuman alipokuwa akifungua mafunzo ya siku nne ya mfumo wa usimamizi wa fedha za umma ujulikanao kama  epicor toleo la 10.2 ulioboreshwa ili kuwawezesha kubadilishana taarifa mbalimbali za fedha,  mifumo ya Mipango na bajeti,  uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma (FFARS) yaliyohudhuriwa na  wahasibu na watunza hazina kutoka  mikoa ya Kagera na Kigoma.

Alisema baadhi ya halmashauri nchini hazitumii mifumo ya fedha iliyopo na wakati huo huo zikishindwa kukusanya mapato na kufanya kazi kwa ufanisi na kuwataka kubadilika na kutumia mifumo iliyopo kwenye halmashauri zao  kikamilifu ili kuboresha ufanisi wa utendaji kazi na miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ya kazi.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo kwa maafisa usimamizi wa fedha kwa Mikoa ya Kigoma na Kagera yanayofanyika Bukoba Mkoani Kagera wakifuatilia mada zilizowasilishwa wakati wa mafunzo hayo jana mjini Bukoba.

" Halmashauri nyingi zimekuwa zikilalamika kukusanya mapato kidogo kutokana na kutokuwa na mifumo, lakini ipo baadhi ya mifumo, ukiwemo mfumo wa Poss ambao hautumiki ipasavyo, na vifaa vya kusaidia mfumo huo vipo", alisema na kuushukuru Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za umma (PS3) kwa ufadhili wa mafunzo hayo ambayo yanaendeshwa na wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Alisema mafunzo hayo ya mfumo wa Epicor 10.2 ambao umeboreshwa, yanayoendelea  kwa mikoa ya Dodoma, Mwanza, Mtwara na Iringa  yana lengo la kuwapa washiriki uelewa wa mabadiliko na maboresho yaliyofanyika kwenye mfumo   ili wafanye  kazi zao kwa ufanisi.

Aliwataka watalaam wanaopatiwa mafunzo hayo kuhakikisha wanayatumia kikamilifu ili kuleta ufanisi wa kazi za kimfumo kwenye halmashauri zao na wasiendelee kutoa visingizio vya mifumo kutofanya kazi na aliahidi kufuatilia mwenyewe jinsi watakavyokwenda kutekeleza majukumu yao.

" Sisi ndio viongozi ambao tunategemewa kufanikisha mifumo hii na raslimali zimetengwa kwa ajili ya kutukusanya hapa, hivyo lazima tuhakikishe mafunzo haya tunayatumia vizuri", alisema.

Meneja wa mradi wa PS3 mkoa wa Kagera Bw. Henry  Shishira akifuatilia hotuba ya Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Bw. Diwani Athumani wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo kwa maafisa usimamizi wa fedha kwa Mikoa ya Kigoma na Kagera yanayofanyika Bukoba Mkoani Kagera.

Alisema miaka sita iliyopita, serikali kupitia Tamisemi ilifanya maboresho makubwa kwa kuzingatia epicor toleo la 9.05 kwa halmashauri 133 zilizokuwepo nchini kwa wakati huo, kupitia miundombinu ya Tehama iliyofungwa katika halmashauri chini ya usimamizi wa Kampuni ya Simu ya Taifa, zoezi ambalo liliendelea na kuongezeka halmashauri mpya ambazo pia zilifungiwa epicor toleo la 10.1.

" Mfumo wa Epicor 10.2 umeandaliwa mahususi kuungana na mifumo mingine ili kukidhi matakwa ya maboresho yanayoendelea na yaliyopo ambayo yana lengo la kuwajengea uwezo ili muweze kusimamia mapato na matumizi ya fedha kwenye halmashauri na kuwapatia uelewa wa mabadiliko ya msingi yaliyofanyika bila kukwamisha utoaji wa huduma kwa wananchi wetu", alifafanua.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) Mkoa wa Kagera Henry Shishira alisema kuwa mafunzo hayo ya mifumo yametolewa kwa wakati muafaka ambapo yatawawezesha wahasibu, wakaguzi na watunza hazina kufanya kazi zao kwa ufanisi kwenye halmashauri zao.

Mfumo huo wa Epicor 10.2 unataarajiwa kuunganishwa na mfumo unaowezesha mabenki kulipana nchini (TISS) ambao utaruhusu malipo yote kufanyika kwa njia ya kielektroniki, ambapo pia utahusisha muundo mpya wa uhasibu pamoja na kasima mpya ya mwaka 2014 kama ilivyoelekezwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi