Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mfumo Mpya wa Malipo Serikali za Mitaa Kuboresha Huduma za Jamii
Jun 06, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.

Mfumo wa Malipo Epicor toleo Na 10.2 unatarajiwa kuboresha huduma za jamii  hapa  nchini kama vile afya na elimu kutokana na mfumo huo kudhibiti ufujaji wa fedha katika ngazi zote za Serikali za Mitaa.

Hayo yameelezwa leo, Jijini Dodoma na Mweka Hazina wa Manispaa ya Singida Aminiel Kamnde akiwa ni mmoja wa washiriki wa mafunzo ya mfumo huo, yanayoendelea kutolewa Jiijini humo ambapo Waweka Hazina, Wahasibu, Maafisa Manunuzi, Wakaguzi wa Ndani na Maafisa TEHAMA wanajengewa uwezo wa namna ya kutumia mfumo huo ambao umefanyiwa maboresho makubwa.

“Mfumo wa Epicor 10.2 ni wa uwazi kwa sababu umeziunganisha hata sekta ambazo zinahudumia jamii kama vile afya na elimu. Hivyo basi kutumika kwa mfumo huu jamii itajua ni kiasi gani cha fedha kimetumwa katika kata au kijiji  chake kwa ajili ya masuala ya elimu au afya pamoja na matumizi ya fedha hizo,” amesema Kamnde.

Amesema kuwa, kuna tofauti kubwa kati ya mfumo uliopita epicor 10.1 na mfumo wa sasa epicor 10.2 ambapo awali mfumo huo ulikuwa hauingiliani na mifumo mingine kama vile mfumo wa mapato pamoja na bajeti, lakini mfumo wa sasa umeunganisha mifumo hiyo yote ndani ya mfumo mmoja ambapo imesaidia kuleta uwazi zaidi.

Kwa upande wake, Mhasibu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Luziga Bundala amesema, Watanzania wajipange kuona namna fedha zao zitakavyokuwa zikitumika kupitia mfumo huo mpya ambao utatumika mpaka na watendaji wa vijiji na kata, walimu wakuu pamoja na vituo vya afya.

“Mfumo huu mpya unaonesha uwazi kati ya mapato na matumizi, hivyo hakuna fedha ya Mtanzania itakayopotea kupitia mfumo huu,” amesisitiza Bundala.

Aidha amesema, fedha zote zilizoelekezwa kwenye mashule, vituo vya afya, kata na vijiji sasa zitaonekana katika mfumo huo na matumizi yake yatatakiwa kuingizwa katika mfumo huo yakiambatana na stakabadhi za malipo mbalimbali yaliyofanyika.

Mfumo wa epicor 10.2 unatarajia kuanza kutumika rasmi Julai 1 mwaka huu na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa.

Mwisho….

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi