Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mchengerwa Atoa Ahadi Nono kwa Tembo Worriors
Sep 28, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anafuatilia na anawatakia mema Timu ya Taifa ya Tembo Warriors ambayo Oktoba Mosi mwaka huu wataingia dimbani kuanza kupambania ubingwa wa Kombe la Dunia hapa Istanbul, Ututuki.

Akizungumza kwa njia ya simu na wachezaji hao kutokea Tanzania kupitia kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi ambaye ametangulia hapa Instanbul kuja kuongeza hamasa, Waziri Mchengerwa amesema Serikali ya Tanzania ipo pamoja na wao katika kila hatua na ndio maana Rais ameridhia viongozi wa Wizara kuambatana nao katika fainali hizo.

“Rais na Serikali yenu tupo pamoja na nyinyi, nendeni mkalipiganie Taifa, onesheni uzalendo na kuhakikisha mnarudi na Kombe nchini na hiyo itakuwa ni zawadi kwake Mhe. Rais na Tanzania kwa ujumla”, amefafanua Mhe. Mchengerwa.

Aidha, ameahidi zawadi nono kwa timu hiyo ikiwemo Shilingi milioni 40 endapo watafuzu robo fainali, Shilingi milioni 80 wakifuzu kucheza nusu fainali na Shilingi milioni 100 wakifanikiwa kufuzu fainali za michuano hiyo.

Ameongeza kuwa yeye mwenyewe baadaye atafika Uturuki, pamoja na kuwapa hamasa hiyo anatarajia kufanya mazungumzo na Waziri wa Michezo na kusaini mkataba wa mashirikiano baina ya Tanzania na Uturuki katika sekta za michezo ili kusaidia kukuza sekta hiyo nchini Tanzania.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amewaasa wachezaji hao kuzingatia nidhamu, umoja na kumtanguliza Mungu na kusema kuwa Serikali ipo kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.

Kwa upande wake Nahodha wa  timu hiyo, Steven Manumbu ameahidi ushindi kwa Mhe. Waziri na kusema kuwa timu ipo tayari kwa ajili ya kuipambania nchi yao.

Naye kocha wa timu hiyo, Salvatory Edward amesema morali ya wachezaji hao ipo juu  pia wanatambua nini wanatakiwa kufanya na wanashukuru kwa uwezeshaji wote wa Serikali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi