Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 Zachagiza Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana Kurejeshwa – Naibu Waziri Katambi
Aug 17, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na: Mwandishi Wetu – DODOMA


Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 zimesaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kukusanya Shilingi milioni 847.6 na kuzirejesha serikalini ikiwa ni fedha zilizotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa ajili ya mikopo yenye riba nafuu kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi leo Agosti 16, 2022 wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya uongozi wa Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida yaliyofanyika katika Wilaya ya Bahi, eneo la Sokoni Dodoma.

Mhe. Katambi alieleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka mipango madhubuti ya kuweza kuhakikisha kila mwananchi haachwi nyuma katika ujumuishwi wa uchumi, hivyo wakimbiza mwenge wa uhuru kwa mwaka 2022 wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa ili vijana wengine waweze kunufaika.

“Mbio za Mwenge wa Uhuru si jambo la mzaha, ni ujumbe wa Mhe. Rais na ni jicho katika kuhakikisha maendeleo yanakuwepo. Sasa wewe fanya mchezo utakwenda na Mwenge, usipotekeleza majukumu yako, kupunguza uzembe ubadhilifu, utakufuata na kukuchukulia hatua, hivyo ni vyema kila mmoja akawe makini katika eneo lake,” alisema

Aliongeza kuwa, hadi kufikia Agosti 14 mwaka huu, Mwenge wa Uhuru tayari umeshatembelea jumla ya Halmashauri 135 kati ya 195 zilizopangwa kutembelewa ambapo umefanikiwa kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 941 yenye thamani ya Shilingi bilioni 551.7, kati ya hiyo miradi 64 yenye thamani ya Shilingi bilioni 12.5 ndio iliyobainika kuwa na dosari ikiwemo kukosa nyaraka na changamoto mbalimbali za kiufundi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Katambi amewapongeza wakimbiza mwenge wa uhuru kwa kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika kushiriki Sensa ya Watu na Makazi kwa maendeleo ya taifa.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule baada ya makabidhiano ya Mwenge, alisema Mwenge huo ukiwa ndani ya Mkoa wa Dodoma utakagua miradi 39 na utakimbizwa kwa muda wa siku 8 katika mkoa huu kwenye Halmashauri zote  7.

Akizungumza awali, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Sahil Gelaruma amewataka viongozi wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha miradi yote itakayokaguliwa taarifa ziandaliwe vyema sambamba na kuwa na nyaraka zote muhimu ili kujiepusha na mkanganyiko wakati wa ukaguzi.


Akiongelea kuhusu fedha zilizotolewa na Serikali Kuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kupelekwa katika halmashauri zote nchini kwa ajili ya kutolewa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana, katika Mkoa wa Dodoma jumla ya Shilingi milioni 150 hazijarejeshwa Serikali Kuu.

"Mwenge wa Uhuru unaagiza halmashauri hizo kurejesha fedha hizo haraka kabla mwenge huo haujapita katika halmashauri zao, Mwenge wa Uhuru hautaondoka Dodoma mpaka fedha hizo zitakaporejeshwa, hivyo itakuwa ni jambo la ajabu kwa halmashauri zilizopo makao makuu ya nchi hawatafanikisha hilo," alisisitiza kiongozi huyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi