Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mazingira ni Agenda Inayosaidia Uchumi Kuwa Imara - Waziri Jafo
Feb 07, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muunganona Mazingira), Mhe. Dkt. Selamani Jafo amesema mazingira ndiyo ajenda inayosababisha uchumi kuwa imara.

Amesema hayo wakati akizungumza na wanafunzi kutoka shule mbalimbali, viongozi na wananchi walioshiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la Medeli jijini Dodoma leo Februari 7, 2022.

Zoezi hilo ambalo ni miongoni mwa shughuli zinazofanyika kuelekea uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 unaotarajiwa kufanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango Februari12, 2022.

Pia, Waziri Dkt. Jafo alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kutumia mvua zinazonyeshja katika maeneo mbalimbali nchini kupanda miti ili ikue na hali itakayosaidia katika kurejesha mazingira katika hali nzuri.

Aliwashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza na kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wanafunzi na wananchi kwa ujumla kushiriki katika zoezi hilo.

Aidha, waziri huyo alihamasisha wanafunzi hao kupeleka ujumbe kwa wazazi wao kushiriki katika zoezi la kupanda miti katika maeneo yao ili kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga alisema katika zoezi hilo,wameweza kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda na kivuli.

Bi. Maganga alisema kuwa zoezi hilo limekwenda vizuri na wamejitokeza kwa wingi kushiriki kupanda miti pamoja na kuwepo kwa changamoto ya kuwepo kwa mvua.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi