Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mawaziri wa Sekta ya Nishati wa EAC Wasisitiza Umuhimu wa Kupatikana kwa Nishati ya Uhakika
Feb 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Mawaziri wa Sekta ya Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana leo tarehe 11 Februari, 2022 jijini Arusha kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya hiyo. 

Mkutano huu ulitanguliwa na mikutano ya awali ngazi ya Wataalamu/Maafisa waandamizi uliofanyika tarehe 8 na 9 Februari, 2022 na kufuatiwa na mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 10 Februari 2022.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Januari Makamba ambaye ameambatana na; Katibu Mkuu Wizara yaNishati - Tanzania Bara, Mhandisi Felschesmi Mramba; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini -Zanzibar; Dkt. Mgereza Miraji; Dkt. Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Petroli na Gesi kutoka Wizara ya Nishati; na Maafisa Waandamizi kutokaWizara ya Nishati na Taasisi zake kwaujumla.

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Waziri Makamba aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo nchini. Pia aliwahakikishia kuwa mkutano utafanikiwa kuyafikia malengo yake kufuatia uongozi imara wa Katibu Mkuu wa Jumuiya yaAfrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki.

Vilevile, akaeleza ukanda wa Afrika Mashariki umejaaliwa rasilimali nishati za kutoka hivyo, ni wakati sasa kwa kila nchi kuwa na mikakati imara ya kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana ili kuihakikishia jamii upatikanaji wa huduma zote zinazohitaji nishati.

“Tukiwa tunapitia changamoto za ugonjwa wa COVID-19 tumeshuhudia namna gani nishati zilihitajika katika kusaidia kuleta nafuu na kuokoa maisha ya wananchi wetu”, alisema Mhe. Makamba.

Naye Mwenyekiti wa mkutano huo na Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. Monica Juma alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Wataalamu na Makatibu Wakuu kwa kufanya maandalizi mazuri ya Mkutano huo na kusisitiza kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika ni moja ya viashiria vya kukua kwa uchumi wa nchi yeyote.

Pia akaeleza kukua kwa uchumi husaidia kupunguza utegemezi na hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kuziwezesha Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya uzalishaji wa kutosha viwandani na katika sekta ya kilimo.

Mkutano huu wa 15 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta la Nishati pamoja na mambo mengine utapitia na kutoa maamuzi juu ya; Taarifa ya hali ya utekelezaji wa maagizo ya mikutano iliyopita; Hatua iliyofikiwa hadi sasa katika sekta za Nishati Jadidifu, Nishati ya Umeme na Nishati ya Mafuta; pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Kitaifa na Kikanda ya Sekta za Nishati inayotekelezwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kadhalika, mkutano huu utajadili kwa kina utekelezaji wa mradi wa kituo cha Nishati Jadidifu cha Afrika Mashariki; Mradi wa kufua umeme wa Nsongezi; Mradi wa kufua umeme wa Murongo/Kigagati(14MW) na Taasisi ya Mamlaka ya udhibiti wa Nishati katika Nchi za Afrika Mashariki.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi