Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mawaziri na Naibu Waziri Walioapishwa Kuanza Kazi Mara Moja
Oct 09, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Thobias Robert

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaapishwa Mawaziri saba, Manaibu Waziri 16 wa Wizara mbalimbali pamoja na Katibu mpya wa bunge aliowateua hivi karibuni.

Hafla hiyo imefanyika leo Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma Spika wa bunge Job Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mawaziri ,viongozi wa Dini, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.

Katika hafla hiyo, Mawaziri walioapishwa ni pamoja na Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe, Wizara ya Nishati Dk. Medard Kalemani, Wizara ya Madini, Angellah Kairuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangalla, Wizara ya Kilimo Dk. Charles Tizeba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo na Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Mkuchika.

Manaibu Waziri walioapishwa ni pamoja na Stella Alex Ikupa Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, William Ole Nasha, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Kangi Lugola, Ofisi   ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Elias John Kwandikwa Ujenzi, pamoja na Mhandisi Atashasta Nditiye Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano.

Wengine walioapishwa ni Dkt. Faustine. Ndugulile Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa Wizara ya Kilimo, Abdala Ulega Wizara ya Mifugo na uvuvi,  Subira Hamis Mgalu Wizara ya Nishati,  Haruni Nyongo Wizara ya Madini,  Ngailonga Josephat Kashunga Wizara ya Maliasili na Utalii, Injinia  Stella Manyanya Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji,   Juliana Shonza Wizara ya Habari, Utamaduni  Sanaa na Michezo, Josephati Kandenge na George Kakunda Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Katika hafla hiyo rais Magufuli pia amemuapisha Bw. Stephen Kagaigai kuwa Katibu wa bunge ambaye amechukua nafasi ya Dkt. Thomas D. Kashilila ambaye atapangiwa kazi nyingine. Kabla ya uteuzi huo Bw. Kagaigai alikuwa Kaimu Karani wa Baraza la Mawaziri. Mawaziri na Manaibu Waziri walioapishwa wametakiwa kuanza majukumu yao mara moja baada ya kumalizika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu mara baada ya kuapishwa.

Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yameongeza idadi ya Mawaziri kutoka 19 hadi 21, na manaibu Mawaziri kutoka 16 hadi 21, ambapo iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini imegawanywa na kuwa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini na iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imegawanywa na kuwa Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Walioachwa katika baraza jipya ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Naibu wake Mhandisi Ramo Makani, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge, pamoja na Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kufanya mabadiliko katika baraza tangu aingie madarakani mwaka 2015, kwani amekuwa akifanya mabadiliko madogo madogo pale inapolazimu ambapo alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye, alitengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani Charles Kitwanga pamoja na kutengua uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi