Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Matumizi ya Teknolojia Yahimizwa Mkutano wa 10 wa Wakaguzi Afrika
Apr 15, 2024
Matumizi ya Teknolojia Yahimizwa Mkutano wa 10 wa Wakaguzi Afrika
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akiwataka wakaguzi wa ndani barani Afrika kutumia utaalam wao wa ukaguzi kuzisaidia nchi zao kutatua chamgamoto, wakati wa Mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Barani Afrika, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Na Peter Haule, WF, Arusha

Wakaguzi wa Ndani barani Afrika wametakiwa kubadilishana uzoefu na kutumia teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali katika taaluma yao na kuhakikisha wanasaidia taasisi na serikali zao kuboresha ufanyaji kazi ili kuchochea maendeleo.

 

Hayo yameelezwa jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, wakati wa Mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Barani Afrika, ulioanza kwa mikutano midogo inayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

 

Dkt. Mkuya alisema kuwa mkutano huo umewakutanisha wakaguzi kutoka nchi 27 za Afrika na kwamba mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu ambapo wageni watajifunza Tanzania na wenyeji watajifunza kwa wenzao kwa kuwa mazingira ya ukaguzi yamebadilika kutokana na kuimarika kwa teknolojia duniani.

 

Mkaguzi Mkuu wa Ndani (IAG), Bw. Benjamini Magai, akizungumzia umuhimu wa ukaguzi kwa maendeleo, wakati wa Mkutano wa 10 wa wakaguzi wa ndani barani Afrika, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

“Tumezoea kuona ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu (CAG) lakini kuna wakaguzi wa ndani ambao wanafanya kazi kila siku ambao husimamia taratibu za matumizi ya fedha, utawala na mifumo hivyo mawanda yao ni mapana katika masuala ya ukaguzi hivyo mkutano huu ni muhimu sana kwa nchi”, alisema Dkt. Mkuya.

 

Alisema Kada ya ukaguzi wa ndani watu wengi hawaielewi hivyo mkutano huo utasaidia kujua mamlaka ya mkaguzi, maadili na taratibu za kufuata ili kuwa na ufanisi katika utendaji kazi.

 

Aidha, Dkt. Mkuya alisema mkutano huo utafuatiwa na mkutano Mkuu utakaofunguliwa Aprili 17 mwaka huu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.

 

Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Ukaguzi Tanzania (IIA Tanzania), Dkt. Zelia Njeza, alisema kuwa mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Afrika umehudhuriwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Ukaguzi Duniani (IIA Global) ambao kabla ya mkutano huo wa 10 walikuwa na kikao chao cha Bodi, jijini Arusha.

 

Alisema kuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya IIA Grobal kuwa na mkutano wao wa Bodi Afrika, hivyo Tanzania inajivunia kupata ujio huo ambao una faida kwa kada ya ukaguzi lakini pia katika sekta ya utalii.

 

Dkt. Zelia alisema kuwa mkutano huo unategemea kuwa na washiriki zaidi ya 1,000 na kati yao washiriki 300 ni wageni kutoka nchi za Afrika na nje ya Afrika.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum (wa tano kushoto), Mwenyekiti wa Taasisi ya Ukaguzi Afrika, Bi. Ruth Mutebe (wa sita kulia), Rais wa Taasisi ya Ukaguzi Tanzania, Dkt. Zelia Njeza (wa sita kushoto), Mkaguzi Mkuu wa Ndani (IAG), Bw. Benjamini Magai (wa nne kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani Duniani na wajumbe wengine, wakati wa mkutano wa 10 wa wakaguzi wa ndani Afrika, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Alisema mkutano Mkuu wa Wakaguzi utafanyika kwa siku tano ambapo umeanza na mkutano wa Jukwaa la Viongozi kutoka taasisi za umma na binafsi ambao wengi ni Wakurugenzi wa Bodi, Taasisi na Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi wa Ndani.

 

Dkt. Zelia alisema kuwa, mkutano huo utasaidia kubadilishana mawazo na kuwa sauti ya pamoja ya kada ya wakaguzi katika kutatua changamoto mbalimbali na kuzisaidia nchi za Afrika kuongeza kasi ya maendeleo.

 

Aidha alizitaja mada zitakazowasilishwa kuwa ni pamoja na mazingira, utawala bora na uadilifu, ambapo alisema mada hizo zitaenda sambamba na majadiliano yatakayoondoa kufanya kazi kwa mazoea na kuwa na sauti moja ya wakaguzi kwa kufanya kazi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

 

Mkutano kama huo wa Wakaguzi Afrika ulifanyika nchini Zambia mwaka 2022 na katika mkutano huo Tanzania ilifanikiwa kushinda kuwa mwenyeji wa mkutano wa 10 baada ya kushindanishwa na nchi nyingine barani Afrika.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi